2013-12-05 08:23:13

Mahubiri wakati wa Kipindi cha Majilio kuongozwa na tafakari kuhusu Mtakatifu Francisko wa Assisi


Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu wakuu na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za Kitume, kuanzia Ijumaa tarehe 6 Desemba, 2013 wanashiriki katika mahubiri ya Kipindi cha Majilio yanayotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri mkuu wa nyumba ya kipapa. Mada inayoongoza mahubiri haya ni "kuelekea Noeli ya Bwana pamoja na Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alifanya hija ya kichungaji mjini Assisi na kauli mbiu itakayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu ni "udugu ni msingi na njia ya amani". Padre Cantalamessa anasema, hii ni fursa kwa Mama Kanisa kutafakari tena na tena mchango endelevu uliotolewa na Mtakatifu Francisko wa Assisi katika maisha na utume wa Kanisa, hasa wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anapoendeleza mchakato wa mabadiliko yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Ijumaa, tarehe 6 Desemba 2013, Baba Mtakatifu na wale wote watakaohudhuria mahubiri haya kwa pamoja watatafakari kuhusu: Mtakatifu Francisko wa Assisi na mageuzi ndani ya Kanisa kwa njia ya utakatifu wa maisha. Ijumaa tarehe 13 Desemba, mada itakaoongoza tafakari kwa siku hiyo ni: Unyenyekevu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi njia ya Kiinjili katika kudumisha udugu na amani. Ijumaa tarehe 20 Desemba, mada itakuwa ni: Mtakatifu Francisko mbele ya Fumbo la Umwilisho: ufukara wa Kristo na ule wa Mtakatifu Francisko.







All the contents on this site are copyrighted ©.