2013-12-05 12:08:56

Kanisa halina sababu ya kuogopa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano!


Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei limeanza mkutano wake wa ishirini na sita kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya walei, unaoongozwa na kauli mbiu "Kumtangaza Kristo katika kipindi cha digitali". Katika mahubiri yake amewataka wajumbe hawa kuhakikisha kwamba, wanajenga maisha yao ya Kikristo katika mwamba thabiti ambaye ni Yesu Kristo, kwa kufuata maamuzi thabiti ya maisha pamoja na kutekeleza mapenzi ya Mungu.

Kardinali Rylko anasema kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi watu wengi wanapenda maisha ya mkato ambao hayajengwi katika msingi thabiti, lakini waamini wanaalikwa kujenga matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya amani na furaha ya kweli. Huu ni mwaliko wa kupokea, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele vya maisha, ili liwe ni dira na mwongozo wa maisha.

Mama Kanisa anatumwa kuwatangazia watu wa kizazi cha dijitali ujumbe wa amani na matumaini kwa kutumia njia mbali mbali za mawasiliano ya jamii, sanjari na kutambua kwamba, njia hizi zina mafao yake makubwa, lakini wakati mwingine zina vivuli na giza linaloweza kuwapoteza watu. Wakristo wawe makini katika matumizi ya njia za mawasiliano ya kijamii kwa kuonesha utambulisho wao unaojikita kwa njia ya majadiliano ya kina; kwa kuhamasisha na kutia moyo pasi na kukata tamaa.

Ulimwengu wa dijitali anasema Baba Mtakatifu Francisko ni changamoto ya kimissionari kwa Wakristo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ili kuwasaidia watu waweze kukutana na Yesu anayezima kiu ya undani wa maisha yao. Ili kukabiliana na changamoto hii, kuna haja ya kuwa na majiundo makini kwa waamini walei ambao ni wadau wakuu na watumiaji wa mitandao ya kijamii katika maisha yao ya kila siku.

Ikumbukwe kwamba, ulimwengu wa dijitali unaundwa na wanawake na wanaume, wanaobeba ndani mwao: matumaini, mahangaiko na wasi wasi wa maisha. Ni watu wanaotafuta kilicho cha kweli, kizuri na chema. Lakini ikumbukwe kwamba, kila mtu binafsi anaalikwa kukutana na hatimaye, kuambatana na Yesu katika hija ya maisha yake. Kutokana na ukweli huu, njia za mawasiliano ya kijamii hazitoshi kufikisha ujumbe wa Injili katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; mtu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kila Mkristo anapaswa kuhamasika kuwa ni mtangazaji wa kweli za Kiinjili.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Kardinali Rylko amempongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa utume na maisha yake, lakini kwa maamuzi machungu aliyoyachukua kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Ni kiongozi aliyewahamasisha waamini walei kutekeleza wajibu na dhamana yao katika maisha na utume wa Kanisa, wakitambua kwamba, wanatumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji!

Wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuridhia tena Baraza la Kipapa kwa ajili ya waamini walei kuendelea na utume wake. Amegusia kuhusu Kongamano la Waamini walei lililofanyika Younde, nchini Cameroon, Septemba 2012, kama sehemu ya mchakato wa majiundo ya waamini walei ili waweze kuyafahamu vyema Mafundisho ya Kanisa, tayari kuyatolea ushuhuda, wakitambua kwamba, wao wanapaswa kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa.

Awamu ya Pili ya Sinodi ya Afrika na Sinodi ya Uinjilishaji Mpya sanjari na Mwaka wa Imani ni matukio ambayo yamekuwa na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Siku ya Vijana Duniania kwa Mwaka 2013 imekuwa na mafanikio makubwa inayowataka vijana kuendelea kuwa ni watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Maadhimisho haya ni sehemu ya mchakato wa majiundo makini kwa vijana, yaliyoanzishwa kunako mwaka 1985 na Mwenyeheri Yohane Paulo II. Mwaka 2016, Vijana watakusanyika Jimbo kuuu la Cracovia, Poland.

Kardinali Rylko anasema, wanawake kwa njia ya semina mbali mbali wameendelea kujengewa uwezo ili kutambua dhamana na mchango wao wa kimama katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani amekutana na vyama mbali mbali vya kitume, akivitaka kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kusoma alama za nyakati; kwa kuwa na ari pamoja na mbinu mpya kwa ajili ya watu wa kizazi hiki. Huu ni wajibu unaofumbatwa kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo.

Njia mpya za mawasiliano ni nyenzo muhimu sana kwa Kanisa katika kuwafikia watu wengi zaidi, lakini kwa namna ya pekee vijana ambao wanatumia muda wao mwingi katika mitandao ya kijamii. Vijana hawa watangaziwe Kweli za Kiinjili; wajengewe jukwaa la majadiliano ili kuondoa wasi wasi na hatimaye, kuimarisha matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kusikiliza, kujadili na kuimarishana ili kutafuta mambo msingi katika maisha.

Tafiti za kitaalam zinaonesha kwamba, kuna matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yanayofanywa na vijana kwa ajili ya: masomo, mawasiliano, michezo na kwamba, kuna baadhi ya vijana wamejikuta wakitumbukia katika hatari za kumezwa na malimwengu yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Kanisa linapaswa kuonesha uwepo wake wa kinabii kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji. Hakuna sababu ya kuogopa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, kwani kati ya zawadi kubwa ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia watu wa nyakati hizi ni njia mpya za mawasiliano ya kijamii.

Yesu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mchakato mzima wa Uinjilishaji kama njia ya kuwashirikisha wengine ujumbe wa matumaini, neema na upendo wa Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.