2013-12-05 09:01:46

Hija ya amani, upendo na mshikamano wa dhati na Wakristo Mashariki ya Kati!


Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vaticani pamoja na ujumbe wake, wamehitisha hija ya kichungaji waliyoianza tangu tarehe 29 Novemba hadi 3 Desemba 2013 nchini Jordani kwa kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa na Serikali, kama sehemu ya mchakato wa kutaka kuimarisha mshikamano kati ya Yordani na Vatican kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi, kudumisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu.

Ametembelea na kukagua miradi mbali mbali inayofanywa na Wakristo nchini Yordani pamoja na maeneo muhimu ya kihistoria. Amezungumza na wafanyakazi wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Yordan ambalo kwa sasa liko mstari wa mbele kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kutokana na vita na kinzani za kijamii zinazoendelea huko Mashariki ya Kati.

Katika hija hii ya kichungaji, Askofu mkuu Mamberti amewahakikishia waamini na wananchi wa Yordan katika ujumla wao, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wao kwa njia ya sala. Viongozi wa Yordan wanasema, wanatarajia kuonana na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Israel panapo majaliwa. Wamepongeza uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Yordan bila kusahau mchango wa Wakristo katika ustawi na maendeleo ya wananchi walioko Mashariki ya Kati.

Ni matumaini ya Vatican kwamba, amani na utulivu vitaweza kurejea tena huko Mashariki ya Kati na kwa namna ya pekee nchini Syria ambako kuna maelfu ya watu wanaoendelea kuteseka. Vyombo vya habari nchini Yordan vimetafsiri hija hii ya kichungaji iliyofanywa na Askofu mkuu Dominique Mamberti kuwa ni ujumbe wa amani na mshikamano pamoja na kuwatia shime Wakristo Mashariki ya Kati kuendelea kutolea ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake.

Hija ya kichungaji itakayofanywa na Baba Mtakatifu huko Mashariki ya Kati, itakuwa ni kikolezo kingine cha kuwatia shime kusonga mbele kwa matumaini makubwa zaidi, licha ya majanga wanayokabiliana nayo!







All the contents on this site are copyrighted ©.