Papa Francisko kutembelea Hospitali ya Bambino Gesù ili kusalimiana na watoto wagonjwa
hapo tarehe 21 Desemba 2013
Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, amewashukuru wanamuziki na wageni
mbali mbali walioshiriki katika tamasha la muziki kwa ajili ya kuchangia gharama za
ukarabati na ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa
na kuendeshwa na Vatican. Hospitali hii ni kielelezo cha mshikamano wa dhati unaoneshwa
na Mama Kanisa kwa watoto wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Askofu
mkuu Parolin anasema, watu wenye karama na vipaji kutoka medani mbali mbali za maisha
wanaweza kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuwaonjesha wengine huruma na upendo,
kwa njia ya kuwajengea madaktari na wauguzi uwezo na nyenzo zinazowawezesha kutoa
huduma makini na za kisasa kwa watoto wagonjwa. Hospitali ya Bambino Gesù haina budi
kuonesha mazingira ya ukarimu na huruma kwa watoto wagonjwa pamoja na wazazi na walezi
wanaowahudumia wanapokuwa Hospitalini hapo.
Kutokana na kuguswa na mateso pamoja
na mahangaiko ya watoto wagonjwa, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa Jumamosi, tarehe
21 Desemba 2013 kuwatembelea watoto wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Bambino
Gesù iliyoko mjini Roma. Jamii bora inapimwa kwa huduma makini inayotolewa kwa wanyonge
na wagonjwa.
Hija hii ya kichungaji kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake,
Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaonjesha watoto wagonjwa huruma na upendo unaobubujika
kutoka kwa Mama Kanisa, kama sehemu ya mchakato unaopania kuwajengea watoto hawa matumaini
ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Wadau mbali mbali wanaendelea kuhimizwa kuboresha
huduma kwa watoto wagonjwa kwani huu ni utume unaobubujika kutoka katika Injili ya
Furaha.