2013-12-04 11:42:07

Balozi wa Vatican aanza utume wake rasmi nchini Uganda


Askofu mkuu Michael August Blume, Balozi wa Vatican nchini Uganda, hivi karibuni amewasili nchini Uganda, tayari kuanza utume wake kama Mwakilishi wa Vatican nchini Uganda. Kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebe, Uganda, amepokelewa na viongozi wa Serikali na Kanisa. Askofu mkuu John Baptist Odama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda alimkaribisha na kumwonjesha ukarimu kutoka kwa watu wa Afrika ya Mashariki.

Tarehe 3 Mei, 2013, Askofu mkuu Blume aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa viongozi wa Serikali ya Uganda chini ya uongozi wa Bwana Henry Oryem Okello, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Tarehe 4 Juni 2013, kwa mara ya kwanza akafungua mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda sanjari na kuwasilisha barua zake za utambulisho kutoka kwa Katibu mkuu wa Vatican, wa wakati huo Kardinali Tarcisio Bertone.

Tarehe 15 Novemba 2013, Askofu mkuu Michael August Blume akiambatana na Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa nchini Uganda, walikagua gwaride la heshima, lililoandaliwa kwa heshima ya Askofu mkuu Blume na baadaye, akiwa anasindikizwa na Askofu mkuu Charles Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala, walikutana na kuzungumza na Rais Yower Kaguta Museveni wa Uganda.

Katika mazungumzo yao, waligusia umuhimu wa kulisimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; maisha dhidi ya utamaduni wa kifo mambo ambayo kimsingi yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika mila na desturi za wananchi wa Uganda. Rais Museveni amelipongeza Kanisa kwa kuendelea kutetea zawadi ya maisha; umuhimu wa Uinjilishaji Mpya; haki, amani na upatanisho; mambo msingi yaliyobainishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika, Africae Munus.







All the contents on this site are copyrighted ©.