Ujumbe wa amani na matumaini kwa wananchi wa Sudan ya Kusini
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani imekuwa ni nafasi kwa waamini kujikumbusha kwamba, wanaitwa
na kutumwa kila siku na Yesu Kristo ili kutangaza Injili ya furaha hadi miisho ya
dunia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Maaskofu wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu
wanahimizwa kuwaimarisha ndugu zao katika misingi ya imani, maadili na utu wema, daima
wakipania kujenga umoja na mshikamano thabiti ndani ya Kanisa na kati ya watu wa mataifa.
Hii ni sehemu
ya ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Sudan, mara baada ya kufunga Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani. Wanasema, Kanisa linaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Yohane
wa XXIII alipochapisha Waraka wa Kichungaji, Amani Duniani, Pacem In Terris,
kwa ajili ya Watu wote wenye mapenzi mema. Ni waraka unaokazia: haki na amani inayopatikana
kwanjia ya majadiliano ya ushirikiano kati ya watu; amani kama kikolezo cha maendeleo;
hati na dhamana ya watu ndani ya Jamii sanjari na mafao ya wengi. Waraka huu unabubujika
utajiri wa Kiinjili unaofumbata tunu msingi za kiutu zinazohifadhiwa kwenye sakafu
ya mioyo ya binadamu. Ni Waraka unaoonesha sauti ya kinabiii inayotolewa na Mama Kanisa
kwa watu wa nyakati hizi, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuweza kuwa
kweli ni watu wapya ndani ya Kristo. Maaskofu wanaendelea kusema kwamba, wananchi
wa Sudan ya Kusini wanfurahia sasa demokrasia na amani; wanaendelea kujenga na kuimarisha
moyo wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa kushirikiana katika kutafuta mafao
ya wengi nchini Sudan ya Kusini. Hata pale wanaposigana bado kuna matumaini na mwelekeo
chanya wa kuweza kupata suluhu ya kudumu. Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini wanasikitika
kusema kwamba, rushwa, upendeleo na ukabila ni kati ya mambo yanayosababisha kero.
Kuna haja ya kuimarisha misingi ya ukweli na uwazi, huduma na mafao ya wengi pamoja
na kubainisha vipaumbele vichache vinavyoweza kutekelezeka kwa ajili ya maendeleo
ya watu. Wananchi wajitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa,
kinzani na migogoro inayojitokeza miongoni wa mwa wananchi wa Jonglei ni jambo lisilokubalika
kamwe, kwani Sudan ya Kusini inajengwa na watu kutoka katika kila kabila, lugha na
jamaa. Wananchi wa Jonglei wanahimizwa kusimama kidete kulinda na kutetea misingi
ya amani na kwamba, Kanisa liko pamoja nao! Maaskofu wanasema kuwa uhusiano kati
ya Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini si mzuri sana, kumbe, kuna haja ya kuendeleza jitihada
za makusudi ili kujenga na kuimarisha uhusiano katika nyanja mbali mbali za maisha
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan katika ujumla wake. Wananchi
wanaorudi Sudan ya Kusini baada ya vita na kinzani za kijamii, waonjeshwe ukarimu
na upendo, ili waweze kuanza tena maisha mapya. Maaskofu Kusini mwa Sudan wanasema,
tatizo la Jeshi la Waasi kutoka Uganda pamoja na suala la Abyei ni mambo nyeti yanayopaswa
kushughulikiwa kikamilifu ili: haki, amani, utulivu na maendeleo ya kweli yaweze kupatikana.
Mchakato huu uwe ni sehemu ya mikakati ya uponyaji na upatanisho nchini Sudan ya Kusini;
mchakato ambao unawahusisha wadau mbali mbali nchini Sudan. Maaskofu wanaipongeza
Tume ya Kitaifa ya Uponyaji, Amani na Upatanisho na kwamba, wataendelea kuunga mkono
juhudi hizi kwa kupitia Tume ya Haki na Amani.