2013-12-03 07:38:49

Simameni kidete kulinda na kutetea familia kwani ni kwa ajili ya mafao ya wengi!


Shirikisho la maisha ya Familia Barani Afrika, lililowakutanisha wajumbe kutoka katika vyama vya kitume 28 vinavyowakilisha nchi 22 , limehitimisha kongamano lake la tatu kimataifa chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM na kuhudhuriwa na Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki Cor Unum. Mkutano huu ambao umefanyika nchini Mauritius kwa kuongozwa na kauli mbiu “Familia kama mafao ya wengi; tusimame kidete kuilinda”. RealAudioMP3

Shirikisho hili linapata chimbuko lake katika Mafundisho ya Mababa wa Kanisa kwa kutambua kwamba, familia ni msingi wa maisha ya binadamu, jamii na Kanisa katika ujumla wake na kwamba, maendeleo na ustawi wa jamii kwa siku za usoni unategemea kwa kiasi kikubwa familia.

Katika kongamano la siku tatu, wajumbe pamoja na mambo mengine waliangalia: vitisho dhidi ya utu na heshima ya binadamu; utekelezaji wa mikakati ya Cairo kuhusu sera za maendeleo kwa Mwaka 2013 na baadaye mintarafu Bara la Afrika. Mikakati ya kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya kifamilia dhidi ya utandawazi; familia na majiundo ya mtu; mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke; umuhimu wa kutunza usafi wa moyo; changamoto za useja katika maisha ya kifamilia; huduma ya maisha katika utume wa familia.

Wajumbe wamevipongeza vyama vya kitume kwa ajili ya familia vinavyojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya katika mchakato wa kupambana na mmong’onyoko wa maadili na utu wema pamoja na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi, bila kusahau maandalizi kabla ya ndoa.

Wanandoa wanapenda kutoa changamoto kwa SECAM kuhakikisha kwamba, inasaidia kwa hali na mali majiundo ya wahudumu wa maisha ya ndoa na familia, ili kusaidia kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mapenzi ya Mungu, mafao ya familia kwa kukumbatia Injili ya Uhai. Familia ni mahali panapoonesha ukarimu wa kuwapokea na kuwalea watoto; ni jukwaa makini la malezi kwa watoto na mahali pa kurithisha tunu bora za maisha. Hii ni kanuni msingi kwa wana chama wa Shirikisho hili.

Washiriki wa kongamano hili wanalipongeza Kanisa kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utamaduni wa maisha na familia na kwamba, kama Waafrika, wanathamini sheria asilia za maumbile, maisha ya binadamu, jumuiya na familia na kwamba, wanathamini mila na desturi njema zisizosigana na Injili. Wanaitaka Familia ya Mungu Barani Afrika kuwa makini dhidi ya vitisho vinavyojitokeza katika maisha ya ndoa na familia.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni kati ya mambo yanayotaka kupelekea baadhi ya Jamii za Kiafrika kukengeuka kwa kuacha misingi ya maadili na utu wema kama njia ya kupata fedha na misaada, jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika! Watu wasimame kidete kutetea na kulinda familia dhidi ya sera dhidi ya ongezeko la watu zilizopitishwa kwenye mkutano wa idadi ya watu kimataifa, uliofanyika mjini Cairo kunako Mwaka 1994 sanjari na Itifaki ya Maputo.

Wajumbe wa Kongamano la Shirikisho la Maisha ya Familia Barani Afrika wanasema, wanapenda kusimama kidete kumwilisha kwa umakini mkubwa mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia na kamwe, watu wasikubali kukengeuka dhidi ya tunu msingi za maisha, utu na heshima ya binadamu, kwani familia kadiri ya mapokeo, mila na tamaduni nyingi za Kiafrika ni madhabahu ya upendo, maisha na tumaini la mwanadamu kwa siku za usoni.

Wajumbe wanaipongeza SECAM kwa sera na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya familia Barani Afrika. Wanaomba Mabaraza ya maaskofu mahalia kuhakikisha kwamba, Makleri wanapata majiundo makini kwa ajili ya ndoa na familia wanapokuwa kwenye malezi; Kanisa liendelee kushirikiana na wanasiasa wanaotetea na kusimamia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na thamani ya maisha katika maeneo yao na kamwe wasichoke kulinda na kuitetea familia.

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.