Mwaka wa Uinjilishaji Mpya unapania kuwaonjesha watu Injili ya Furaha kwa kukutana
na Kristo!
Maadhimisho ya Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio, Jimbo kuu la Castries nchini
Antille ni mwanzo wa Mwaka wa Uinjilishaji Mpya unaopania kuchochea mwamko wa utangazaji
wa Injili ya Furaha miongoni mwa wananchi wa Saint Lucia.
Ni mwaliko kwa waamini
kuwaonjesha jirani zao huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya ujio wa
Yesu Kristo Masiha na Mkombozi wa dunia. Ni mwaliko wa kuimarisha imani kwa Yesu Kristo
Mwana wa Mungu aliye hai na kwamba, wote wanakaribishwa kushiriki katika karamu ya
upendo inayoandaliwa na Kristo mwenyewe.
Kanisa kwa asili ni la Kimissionari,
utume ambao unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, changamoto ya kuimarisha
umoja na mshimano wa Kikanisa na kwamba, kila mwamini anachangamotishwa na Mama Kanisa
kushiriki kwa ukamilifu katika dhamana hii, hasa katika ulimwengu wa utandawazi, unaotaka
kumng'oa Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu.
Ni mahubiri yaliyotolewa
na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu
wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Antilles, iliyoko kwenye Visiwa vya Caribbean
sanjari na uzinduzi wa Mwaka wa Uinjilishaji Mpya, unaowasukuma waamini kutolea ushuhuda
wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; wakiwamegea wengine Injili ya Furaha inaojikita
katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Waamini waitambue imani yao
na kujitahidi kuwashirikisha wengine kwa kuwaendea hasa wale walioko pembezoni mwa
Jamii, ili nao waweze kuonja na kuguswa na upendo wa Kristo kwa njia ya waamini. Uinjilishaji
ni dhamana endelevu kwa Wakristo wa nyakati zote kutokana na dhamana waliyojitwalia
wakati wa Sakramenti ya Ubatizo na kuimarishwa kwa Kipaimara kwa kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa Kristo ambaye ndiye kiini cha Injili na Imani inayotangazwa na kushuhudiwa
na waamini. Kila mwamini anachangamotishwa na Mama Kanisa kushiriki kikamilifu katika
maisha na utume wa Kanisa.
Kardinali Filoni anapenda kuwahimiza Maaskofu na
wadau wote wa Uenezaji wa Injili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano; kujitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa, hasa zaidi kwa njia
ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Watawa wanahamasishwa
kuwa ni mfano bora wa maisha na tunu za Kiinjili kwa kuishi kikamilifu Mashauri ya
Injili.
Waamini katika ujumla wao, wasimame kidete kulinda na kutetea utu na
heshima ya binadamu; wawe ni watetezi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia
kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na manyofu; daima wakijitahidi kujenga na
kuimarisha Jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano
wa dhati!