2013-12-03 10:48:01

Mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji: changamoto na matumaini yaliyopo!


Wajumbe kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya, CCEE wanaoshughulikia huduma kwa wahamiaji na wakimbizi, kuanzia tarehe 2 hadi 4 Desemba 2013 wanashiriki katika mkutano unaoongozwa na kauli mbiu "Mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na wakimbizi: changamoto na matumaini yaliyopo". Mkutano huu unafanyika mjini Valletta, nchini Malta.

Mabaraza ya Maaskofu Ulaya yanaangalia jinsi ya kushirikiana ili kukabiliana na changamoto za wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na ubora wa maisha Barani Ulaya, kwa kuzingatia utu na heshima yao kama binadamu. Ni fursa ya kupembua tena sera na mikakati kwa wahamiaji na wakimbizi Barani Ulaya.

Kardinali Antonio Maria VegliĆ², Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, akichangia mada kwenye mkutano huu amekazia umuhimu wa utu na heshima ya kila binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na utambulisho wa Wakristo wanaopaswa kuhudumiwa kikamilifu katika maisha yao ya kiroho.

Anasema, wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohitaji kuwa karibu na familia zao kama sehemu ya haki zao msingi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, familia nyingi za wahamiaji na wakimbizi zinakabiliwa na hali ngumu ya maisha pamoja na sera kandamizi dhidi yao, hali inayosababisha upweke na majonzi makubwa. Wakimbizi na wahamiaji wapewe nafasi ya kushirikishwa katika mchakato wa utengamano wa kijamii, kwa kulinda na kutetea haki zao msingi.

Kardinali VegliĆ² anasema, hili ni kundi linalopaswa kuonjeshwa upendo, mshikamano na kupewa huduma msingi ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kutoka katika medani mbali mbali za maisha. Ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima yao kama binadamu; haki na amani, ili watu waweze kupata fursa ya kutulia katika nchi zao wenyewe bila kulazimika kuzikimbia.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi kupata haki zao msingi, kwa kushirikiana na nchi wanamotoka wakimbizi na wahamiaji hao kwa kutambua kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi, Familia ya binadamu inategemeana na kusaidiana. Wahamiaji na wakimbizi wanastahili kupata huduma za maisha ya kiroho, kwa njia ya mshikamano wa upendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.