Maaskofu wasikitishwa na ufisadi ulioitikisa Serikali ya Malawi!
Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari linasema
kwamba, limesali na kufanya tafakari ya kina kuhusu kashfa ya ufisadi wa fedha za
umma unaofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa na uzalendo, kwa kutaka kupata utajiri
wa haraka haraka, kwa njia za mkato, pasi na kuzingatia ukweli, uaminifu, uadilifu
na utendaji wa kazi kwa juhudi, bidii na maarifa.
Maaskofu wanasema, ufisadi
huu umepelekea wizi wa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya huduma
na maendeleo kwa wananchi wa Malawi. Hili ni kundi la watu wasiokuwa na uzalendo ambalo
limeitumbukiza Malawi katika shida na mahangaiko makubwa na kwamba, sera na mambo
ya fedha iko mashakani kutokana na ukosefu wa maadili na ukomavu wa kiutu.
Maaskofu
Katoliki nchini Malawi wanasema, ingawa kashfa hii inashughulikiwa na wadau mbali
mbali, lakini wao pia wanaona kwamba, wanadhamana ya kuweza kuchangia mawazo yao kwa
kuzingatia madhara yanayosababishwa na ufisadi huu unaoendelea kuyatumbukiza mamillioni
ya watu katika umaskini wa hali na kipato, kwa kukosa sera makini zinazotoa kipaumbele
kwa binadamu na maendeleo yake.
Msimamo wa wafadhili kutochangia tena bajeti
ya Serikali ya Malawi, utasababisha madhara makubwa ya kiuchumi kwa ongezeko kubwa
la bei za bidhaa na huduma. Malawi itakosa fedha za kigeni kugharimia huduma mbali
mbali hali ambayo itasababisha majanga kwa wananchi wa kawaida! Ni wananchi ambao
wameporwa fedha zao na kwamba, wataendelea tena kuteseka kwa kukosa huduma msingi
za maendeleo na huduma za kijamii.
Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linasema,
kuna haja kwa Serikali kufanya uchunguzi wa kina na wahusika kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria kujibu shutuma zinazowakabili, ili kujenga tena uaminifu kwa wananchi wa
Malawi pamoja na wafadhili kutoka nje. Serikali ya Malawi ikiri uwajibikaji wake wa
kimaadili na fedha iliyoibwa irudishwe kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Malawi. Serikali iwe makini kusikiliza kilio cha wananchi wa Malawi wakati huu
wa mtikisiko wa uchumi nchini Malawi.
Maaskofu wanawaomba wafadhili kuendelea
kuchangia katika bajeti ya Serikali ya Malawi kwa ajili ya maendeleo ya watu wa kawaida.
Wananchi watubu na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu; wajitahidi kuongozwa na Amri
za Mungu na dhamiri nyofu, tayari kujitoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Malawi. Serikali iwe makini katika kudhibiti fedha ya umma na kuwawajibisha mafisadi
bila huruma. Kanisa liwe mstari wa mbele kuhamasisha moyo wa uzalendo na uwajibikaji.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Malawi linalaani kwa nguvu zote ufisadi, wizi na ubadhirifu wa
mali ya umma unaofanywa na watu wachache waliopewa dhamana ya kusimamia maendeleo
ya watu. Hiki ni kitendo ambacho ni kinyume kabisa cha maadili, changamoto kwa wananchi
wa Malawi, kutubu na kumwongokea Mungu.