2013-12-02 07:39:53

Waraka wa Kitume: Injili ya Furaha: Evangelii Gaudium: kwa muhtasari


Waraka wa Kitume Injili ya Furaha, “Evangelii Gaudium” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya.

Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya anasema, Waraka huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa siku za usoni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi.

Waraka huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko, akayasoma na kuyafanyia tafakari ya kina na hatimaye kuyaweka kuwa ni sehemu ya ujumbe wake kwa Familia ya Mungu wakati huu inapojielekeza katika hija ya Uinjilishaji Mpya, kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ndiye kiini cha Uinjilishaji na ndiye Mwinjilishaji Mkuu. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Yesu mwenyewe katika mazingira mapya ya Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu katika mwono huu wa Kimissionari ambao ndio msingi wa Waraka huu wa kitume anaugawa sehemu kuuu mbili. Sehemu ya kwanza ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kuangalia changamoto na fursa zilizopo mintarafu tamaduni na hali halisi ya nchi husika. Baba Mtakatifu anatoa kigezo kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu na kwa kila mdau wa Uinjilishaji, ili kwa pamoja kuwa na mbinu shirikishi katika mchakato wa Uinjilishaji pasi na kujitenga kama kisiwa!

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha nguzo kuu saba za Uinjilishaji zinazopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mwono wa Uinjilishaji Mpya: Mageuzi ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, Kanisa kimsingi ni la Kimissionari; vishawishi vya Wainjilishaji, Kanisa kama Familia ya Mungu inayotumwa Kuinjilisha; mahubiri na matayarisho yake; ushiriki wa kijamii wa maskini katika maisha na utume wa Kanisa; amani na majadiliano ya kijamii na kiini cha kazi ya Uinjilishaji inayofanywa na Mama Kanisa. Yote haya yanafumbatwa kwa umakini mkubwa katika huruma na upendo mfunuliwa wa Mungu unaogusa moyo wa kila mtu kwa kukutana na Yesu, chemchemi ya furaha inayomsukuma mwamini kushirikisha upendo huu kwa wengine.

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya kwanza ya Waraka wa Kitume: Injili ya Furaha anasema kwamba, mabadiliko yanayopaswa kufanywa na Mama Kanisa ni kutokana na utambuzi kwamba, Kanisa kwa asili ni la Kimissionari, linalofanya hija ya kutoka katika undani wake ili kukutana na Yesu, kwa kutambua kwamba, waamini katika hija hii wanaambatana na Mungu ambaye analionesha Kanisa dira na njia ya kufuata nyayo za Kristo, daima likiwa limesheheni huruma.

Ili yote haya yaweze kutekelezeka, kuna umuhimu wa kuwa na wongofu wa kichungaji unaolitaka Kanisa kuendeleza kazi ya Uinjilishaji kwa kuachana na miundo mbinu ya Kanisa inayoweza kuwa ni kikwazo cha dhamana hii. Wadau wa Uinjilishaji Mpya waoneshe ugunduzi na kuibua mikakati kadiri ya tafiti makini zilizofanywa katika eneo husika, ili kubainisha malengo maalum yanayopaswa kufikiwa na Jumuiya husika kwa kuzingatia mambo msingi tu! Kujenga hierakia za ukweli mintarafu kiini cha Injili inayofumbata upendo. Kunatakiwa kuwepo na uwiano sawa kati ya hazina ya imani na lugha inayotumika, wakati mwingine, lugha inaweza kushindwa kufikisha Kweli za Kiimani.

Baba Mtakatifu katika Sura ya kwanza anawaalika kwa namna ya pekee Waamini kuhakikisha kwamba, wanamwilisha katika maisha na utume wa Kanisa matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican; kuangalia upya dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki hususan katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Wainjilishaji watambue mapungufu yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya lugha ya mwanadamu na kwamba wanapaswa kutambua utajiri unaofumbatwa katika Hazina ya Imani.

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya Pili ya Waraka wa Kitume, Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium, anachambua kwa kina na mapana changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Jambo la msingi ni kuondokana na dhana ya kujisikia wanyonge, hali inayoweza kusababisha Wainjilishaji kushirikisha furaha yao kwa wengine kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Uinjilishaji uwe ni sehemu ya mchakato unaomwezesha mwamini kukua na kukomaa na kwamba, magumu anayokutana nayo yasiwe ni sababu ya kumkatisha tamaa. Wawe makini na matumizi ya teknolojia na utandawazi; kwa kuondokana na mambo yanayosababisha mpasuko wa kijamii kwa kupenda mno fedha na mali; madaraka na heshima; mmong’onyoko wa tunu msingi za maadili na utu wema; soko huria kupewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa halina budi kuendeleza matendo ya huruma na mshikamano kwani hii ni sehemu ya maisha na utume wake miongoni mwa watu wa Mataifa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Uinjilishaji Mpya katika nyakati hizi unakabiliana na changamoto zinazoibuliwa na tamaduni za miji, changamoto kwa waamini kutokubali kumezwa na malimwengu; ukanimungu na mafundisho potofu; imani inayofanya rejea kwa maisha binafsi na kwamba neema inaweza kupatikana kwa kutumia mabavu. Haya yote ni makwazo katika Uinjilishaji mpya, mambo ambayo yanapaswa kung’olewa kabisa kwa kukazia ushuhuda wa umoja unaojionesha kwa kukamilishana. Wanawake na waamini walei wanapaswa kushirikishwa kwa namna ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa, ili waweze kuchangia katika ujenzi wa Kanisa.

Sura ya tatu ya Waraka wa Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium, Baba Mtakatifu anaelezea kwamba, Uinjilishaji ni dhamana ya Familia nzima ya Mungu kwa kutambua neema ya Mungu inayofanya kazi kwa Wainjilishaji wote. Anakazia umuhimu wa kuendeleza utamadunisho kwani Injili haina utambaulisho wa utamaduni maalum sanjari na kukazia mahusiano ya ya kijamii kati ya watu kama njia ya ushuhuda wa Kweli za Kiinjili.

Baba Mtakatifu anawahimiza watu kukuza na kuendeleza Ibada mbali mbali, kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa wale ambao wameonja na kuguswa na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mwishoni mwa surah ii, Baba Mtakatifu anawaalika wanataalimungu kutafuta mbinu mkakati utakaosaidia watu kufurahia njia mbali mbali za Uinjilishaji.

Mahubiri ni sehemu muhimu sana katika Uinjilishaji Mpya, jambo linalohitaji moyo na ari ya kulipenda Neno la Mungu na Watu wa Mungu wanaowahubiria: Mahubiri yawe mafupi na wala yasiwe ni “majigambo” ya kisomi; yawe ni mawasiliano yanayogusa sakafu ya moyo ya mwamini na wala yasiwe ni mahali pa kuwakaripia watu. Wainjilishaji wajiandae kikamilifu, ili mahubiri yao yawaletee watu matumaini na kamwe yasiwatumbukize katika mwono potofu! Neno la Mungu lifundishwe kwa kuwaojengea waamini mwono sahii kwamba linaweza kugusa undani wa maisha yao; linajengeka katika majadiliano, uvumilivu na ukarimu bila ya kuhukumu.

Sura ya nne ya Waraka wa Kitume, Furaha ya Injili, Evangelii Gaudium, Baba Mtakatifu Francisko anaelekezea kwa kina na mapana kuhusu mwelekeo wa uchumi kimataifa unaojikita katika misingi ya ukosefu wa haki, hali ambayo inapelekea wanyonge kuendelea kunyong’onyea katika Jamii na wenye nguvu kufurahia maisha. Utamaduni wa kutojali na kuguswa na mahangaiko ya jirani umeunda kundi kubwa la watu wanaonyonywa na hatimaye, kusukumizwa pembezoni mwa Jamii zao, kama “makapi”. Soko huria ni kati ya nguvu kuu ambayo imeibuka katika Jumuiya ya Kimataifa; watu wanatafuta faida kubwa, rushwa na ufisadi yanaonekana kuwa ni mambo ya kawaida kiasi cha baadhi ya watu kukwepa kulipa kodi kwa makusudi kabisa pamojana na madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo.

Katika sehemu hii, Baba Mtakatifu anaunganish dhamana na umuhimu wa Uinjilishaji pamoja na huduma ya maendeleo kwa mtu mzima, tayari kutolea ushuhuda wa imani katika maisha binafsi na kwenye hadhara. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, analichangamotisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linawahusisha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii katika maisha na utume wake. Kanisa liendelee kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani kwa njia ya majadiliano ya kijamii. Maskini wanayo mengi ya kulifundisha Kanisa na kwamba, kuna haja ya kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya kupambana na umaskini wa hali na kipato miongoni mwa watu.

Anawaalika wanasiasa pia kulivalia njuga baa la umaskini kwa kuwa na sera na mikakati makini kwa ajili ya watu wao. Kanisa ni Jumuiya ya waamini, kamwe hawapaswi kuwasahau maskini wanaoishi nao! Baba Mtakatifu analihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linawahudumia: wakimbizi na wahamiaji; watu wasiokuwa na makazi maalum; wazee wanaotelekezwa na kukumbwa na upweke hasi, ambao idadi yao inaongezeka maradufu. Watumwa wa biashara ya utumwa mamboleo wanapaswa kusaidiwa.

Kuna watu wanaoteseka kutokana na tabia ya baadhi ya watu kukumbatia utamaduni wa kifo na sera za utoaji mimba; hawa ni watu ambao utu wao una nyanyasika. Kuhusu sera za utoaji mimba, Kanisa halitabadili mafundisho yake kwani ni jambo linalokwenda kinyume na zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu na kwamba, hii ni dhamana ya wote.

Baba Mtakatifu anakazia umoja dhidi ya kinzani na mafarakano; ukweli dhidi ya mawazo ya kufikirika; mambo msingi katika mchakato wa majadiliano yanayoweza kusaidia kujenga na kudumisha misingi ya amani katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu: yaani katika masuala ya Kisayansi, Kiekumene na Kidini. Yote hii ni misingi ya Uinjilishaji Mpya ili kujifunza maana kutoka kwa wengine: umuhimu na maana ya mshikamano wa Maaskofu; umuhimu wa Sinodi; haki na amani kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji pamoja na kuachana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, kwani imekuwa ni chanzo cha uvunjifu mkubwa wa amani sehemu mbali mbali za dunia.

Sura ya tano ya Waraka wa Kitume, Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu Roho ya Uinjilishaji Mpya, dhamana inayotekelezwa chini ya usimamizi wa Roho Mtakatifu, anayewawezesha wainjilishaji kujikita katika sala na tafakari ya kina kwa kutambua dhamana na nafasi ya Bikira Maria nyota ya Uinjilishaji Mpya. Mama Kanisa anachangamotishwa katika siku za usoni, kujikita katika azma ya Uinjilishaji Mpya kwa: ari, moyo mkuu na furaha ili kushuhudia upendo endelevu wa Kristo bila kukatishwa tamaa na vizingiti vya maisha. Ni wainjilishaji wanaotekeleza utume wao kwa njia ya Sala na Kazi, ili kumtangaza Yesu Kristo kwa Watu wa Mataifa.

Lugha anayotumia Baba Mtakatifu Francisko inawagusa watu kutoka katika undani wa maisha yao. Mama Kanisa anahimizwa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinaonesha hali halisi katika azma ya Uinjilishaji Mpya, ili Injili ya Kristo iweze kuwafikia watu wengi zaidi, ingawa kuna baadhi ambao wamebahatika kusikia kwa kina zaidi.

Kanisa linatumwa kuwaendea maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii; wagonjwa na wale waliosahaulika. Kanisa lijifunze kutafakari na kumwabudu Mwenyezi Mungu, tayari kumtolea ushuhuda wa imani tendaji. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kutambua kiini cha imani yao kuwa ni Yesu Kristo Mfufuka na Kanisa ambalo linaonesha huruma kwa watu wa nyakati hizi wenye kiu ya kuonana na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Waraka wa Kitume, Injili ya fuaraha, Evangelii Gaudium kwa Sala ya Bikira Maria, Mama wa Uinjilishaji Mpya ambaye kwa mtindo wake wa maisha, Kanisa linapenda kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji. Kila mwamini anayemtaza Bikira Maria awe mshiriki wa mageuzi ya upendo na huruma.

Muhtasari huu umeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.