Waamini wako katika hija ya kuelekea Yerusalemu mpya, mahali ambapo sura ya Mungu
imeonekana na sheria kutangazwa!
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro amewakumbusha waamini kwamba, Kanisa
limeanza Mwaka Mpya wa Liturujia, hija inayofanywa na Watu wa Mungu wakiongozwa na
Yesu Kristo mchungaji mkuu katika utimilifu wa Ufalme wa Mungu. Ni hija inayofanywa
na Mama Kanisa katika wito na utume wake, Familia ya binadamu wote; watu kutoka katika
tamaduni na maendeleo mbali mbali kuelekea katika utimilifu wa nyakati!
Ni
hija ya kiulimwengu kuelekea Yerusalemu mahali ambapo sura ya Mungu imefunuliwa na
Sheria kutangazwa kwa watu wake. Yesu Kristo ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu, ni Neno
wa Mungu aliyefanyika mwili; kiongozi wa hija ya watu wa Mungu anayewaonesha mwanga
unaoelekeza kwenye haki, amani na utulivu. Hakutakuwa tena na vita wala misigano!
Baba Mtakatifu anasema, hii ni hija ya matumaini na amani inayobubujika kutoka kwa
Mwenyezi Mungu na kwamba, ni hija endelevu katika maisha ya mwamini.
Kipindi
cha Majilio ni wakati wa matumaini yasiyodanganya kamwe, kwani Mwenyezi Mungu ni mwaminifu
katika ahadi zake. Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha hija ya maisha, aliyebeba
ndani ya moyo wake matumaini; na tumboni mwake tumaini la Neno wa Mungu aliyefanyika
mwili, yaani Yesu Kristo. Utenzi wa Bikira Maria anasema Baba Mtakatifu ni wimbo wa
mahujaji wanaotumainia: nguvu na huruma ya Mungu.
Mara baada ya Sala ya Malaika
wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbuka wagonjwa wa Ukimwi sehemu mbali mbali
duniani, lakini kwa namna ya pekee, watoto wanaoonja uwepo wa Mama Kanisa kwa njia
ya Wamissionari na wahudumu wa Sekta ya Afya. Baba Mtakatifu amewaombea madaktari
na watafiti waweze kufanikisha kazi yao na kwamba, kila mgonjwa aweze kupata huduma
na asiwepo anayetengwa bila kupata tiba anayohitaji.