Shirikisheni vijana wa kizazi kipya katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi!
Shirikisho la Wakuu wa Shirika la Wayesuit Barani Afrika katika Maadhimisho ya Siku
ya Ukimwi Duniani, kwa mwaka 2013 linaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwahusisha vijana
wa kizazi kipya katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, kwa kuwajengea uwezo,
tunu msingi za kiutu, kijamii na kimaadili pamoja na kuwafahamisha umuhimu wa mchango
wao katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi. Hadi kufikia mwaka 2012 kulikuwa
na jumla ya vijana million mbili nukta moja waliokuwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi
sehemu mbali mbali za dunia.
Mtandao wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi
wa Wayesuit Barani Afrika, AJAN anasema Padre Michael Lewis, Rais wa Shirikisho la
Wakuu wa Shirika la wayesuit Barani Afrika kwamba, wana amini kuhusu ufanisi unaoweza
kupatikana katika elimu makini inayotolewa na AJAN Barani Afrika katika mapambano
dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi; elimu inayotolewa shuleni na kwenye taasisi za elimu.
Vijana wanatambua kwamba, kampeni ya kinga dhidi ya Ukimwi bado haijafanikiwa
sana, kwa mantiki kwamba, huu ni wimbo ambao kwa sasa hauna tena msikilizaji kwani
umezoeleka masikioni mwao na watu wanaendelea kutumbua maisha kana kwamba, hakuna
kinachoendelea duniani kuhusiana na Ukimwi! Wajesuit wanasema, kuna hja ya kuonesha
kipaji cha ugunduzi kwa kuwashirikisha vijana wenyewe katika kampeni dhidi ya ugonjwa
wa Ukimwi.
Vijana waweze kuwa na mawazo pevu na nyenzo za kupambana na Ukimwi,
kwa kuwajibika wanapofanya maamuzi ya maisha, kuwaonesha jirani zao upendo na huruma
pamoja na kufanya maamuzi machungu ya kutaka kubadilika kitabia! Udhibiti wa maambukizi
mapya ya Ukimwi uguse mahitaji ya mtu mzima; mahusiano kati ya mtu na mtu na kati
ya mtu na Muumba wake. Vijana wawe na mitindo mipya ya maisha kwa kufahamu na kuzingatia
mafundisho yanayotolewa na Mama Kanisa.