Nyenzo muhimu za Kipindi cha Majilio: Sala, tafakari na matendo ya huruma!
Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kujiandaa kwa Siku kuu ya Noeli kwa kujikita
zaidi katika Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, toba na wongofu wa ndani, kwani Noeli
ni tukio linalomwezesha mwamini kukutana na Yesu Kristo Masiha.
Ni mwaliko
uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 2 Desemba 2013 wakati wa
Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.
Noeli ni Siku kuu ya kukutana na Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai katika maisha
ya imani, matendo mema na adili, mwaliko wa kumsikiliza Yesu kwa umakini mkubwa, ili
kuonja furaha ya kukutana na Yesu katika hija ya maisha ya kila siku.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini pia kutoa nafasi kwa Kristo ili aweze kukutana nao katika
maisha yao ya kila siku, ili kuwaletea maisha mapya yanayosimikwa katika imani, matumaini
na mapendo. Ili kuweza kukutana na Kristo kuna haja kwa mwamini kuacha moyo wake wazi,
tayari kusikiliza na kutekeleza yale ambayo Kristo anataka kutoka kwa mfuasi wake.
Waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo anamsikiliza mmoja mmoja na wala si kama kundi
la watu tu! Waamini wajitaabishe kukutana na kuonja upendo wa Kristo.
Hija
kuelekea Siku kuu ya Noeli inawawezesha waamini kuwa wadumifu katika: tafakari, sala
na matendo ya huruma ili kuwaonjesha maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii ile Injili ya Furaha