2013-12-02 07:51:11

Mchango wa Kanisa Katoliki katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi duniani


Kanisa linaendelea na hija ya Imani na huduma kwa kujitosa kimasomaso kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi kwa takribani miaka ishirini na mitano iliyopita. Kanisa limeonesha huruma na upendo kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi katika nchi 116 ambazo zimeendelea kupokea misaada kutoka kwa Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki.

Ugonjwa wa Ukimwi umesababisha wasi wasi na majonzi makubwa kwa wahusika wenyewe, familia na jamii katika ujumla wake: magonjwa na kifo ni mambo ambayo yako daima mbele ya nyuso zao!

Ni maneno ya Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada Kimataifa, Caritas Internationalis wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, inayoadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe Mosi Desemba. Miaka saba iliyopita, Caritas Internationalis imeanzisha kampeni ya kupambana ili kuutokomeza ugonjwa wa Ukimwi, ili kudhibiti maambukizi mapya na kuondokana na unyanyapaa unaojitokeza katika jamii.

Lengo hili linaweza kufikiwa ikiwa kama kutakuwa na uwajibikaji katika mahusiano kati ya watu; mabadiliko ya tabia na kuwa waaminifu kwa tendo la ndoa ambalo kimsingi ni kwa ajili ya watu wa ndoa na wala si mahali pa kujirusha! Ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Watu wawe na ujasiri wa kupima afya zao mara kwa mara pamoja na kuzuia maambukizi mapya kutoka kwa Mama kwenda kwa mwana, kampeni inayofanyiwa kazi na Jumuiyaya Kimataifa kwa sasa.

Kwa njia ya mshikamano wa umoja, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, kwani Zaidi ya waathirika million kumi kutoka katika nchi zinazoendelea duniani wameweza kupatiwa huduma ya dawa za kurefusha maisha. Idadi hii ni ndogo ikilinganishwa na watu million kumi na nane wanaohitaji kupata huduma ya dawa za kurefusha maisha.

Inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya wafadhili wameanza kupunguza misaada yao katika tiba kwa kile kinachodaiwa kwamba, wamechoka kusaidia! Serikali husika kwa sasa zinatakiwa kubeba dhamana ya kuwahudumia watu wake hasa wakati huu wa athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Caritas Internationalis inakumbusha kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi, kuna mwingiliano mkubwa sana wa watu na dunia kwa sasa ni kama kijiji, kumbe, kuna haja ya kutegemezana na kujenga mshikamano wa udugu na upendo miongoni mwa familia ya binadamu.

Inasikitisha kuona kwamba, bado watu walioathirika kwa Ukimwi wananyanyapaliwa, Kanisa litaendelea kufanya hija ya Imani, Matumaini na Huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi hadi kieleweke, likijitahidi kuiga mfano wa watakatifu mbali mbali waliojisadakisha kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa waliokuwa kufani, kwa kutambua kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kila mtu ana thamani mbele ya mwenyezi Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.