2013-12-02 08:36:21

Kanisa la Nyumbani! Familia iwe ni daraja la kwenda mbinguni!


“Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu”. Ebr. 13:4a. Mpendwa msikilizaji, neno hili elekezi, litatuongoza katika tafakari zetu zote za Kipindi chetu hiki cha Kanisa la Nyumbani. Kukuletea kipindi hiki, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB kutoka Abasia ya Roho Mtakatifu Mvimwa – Sumbawanga, Tanzania. RealAudioMP3

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, wanatutafakarisha juu ya Familia kama Kanisa la nyumbani. Mafundisho ya imani yetu yanatuelekeza kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya jumla ya ukombozi. Ni kwa namna hiyohiyo,Familia ya Kikristo ambayo ni Kanisa la nyumbani, nayo tunaitazama kama Sakramenti, yenye lengo lilelile la kumkomboa mwanadamu mwili na roho.

Hapa, tunataka kusema, familia ziwe ni chombo cha kumuunganisha mwanadamu na mwanadamu mwenzake na hatimaye mwanadamu huyu aunganike na Muumba wake. Kifupi tunataka kusema FAMILIA ZETU ZIWE DARAJA YA KWENDA MBINGUNI.

Katika mfululizo wa vipindi vyetu “Kanisa la Nyumbani”, tutatafakari kwa kina juu ya maana, hadhi, uzito na wajibu wa kila mmoja katika kulijenga Kanisa la nyumbani. Mama Kanisa Mtakatifu anatualika kuienzi tunu hii ya maisha ya familia, ili kutoka kwayo, Kanisa lizidi kusitawi na jamii nzima ya mwanadamu iendelee kujengwa katika roho ya utu na heshima kwa Mungu.

Tunapoongea juu ya familia katika Kanisa, moja kwa moja tunagusa suala msingi la Sakramenti ya ndoa. Kristo Yesu, aliinua ndoa kuwa sakramenti, na akaesema “alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asitenganishe”. Kwa maneno hayo ndipo haswa alipothibitisha misingi na hadhi ya agano la ndoa. Muasisi wa Sakramenti ya ndoa ni Mungu mwenyewe.

Kabla hatujazama ndani kabisa ya mada yetu; ni vema sote tujue kwamba, ndoa ni wito. Humo wanaingia tu wale walioitwa katika maisha ya ndoa. Ni Mungu mwenyewe ndiye anayeita na sisi wanadamu kwa unyenyekevu na imani, tunaitika wito huo na kukubali wajibu zake; yaani kudumisha upendo, kuzaa watoto na kuwatunza. Na ni katika kuupokea wito huo na wajibu zake ndipo tunapolijenga KANISA LA NYUMBANI.

Kwa vile Sakramenti ya ndoa ni wito, ni vema kuupokea wito huu kwa umakini mkubwa. Na kisha kuupokea wito huu kama ilivyo kwa miito mingine, ni vema kuendelea kuuitika kila siku kwa njia ya kuomba neema ya udumifu, kutimiza wajibu na kudumisha upendo wa kujisadaka kwa ajili ya mwenzi na kwa ajili ya usitawi wa familia.

Baada ya kuuadhimisha mwaka wa Imani, kazi itakayobaki mbele yetu, ni kuitambua kwa dhati na kuiimarisha misingi ya Kanisa. Na moja ya tunu kubwa za Kanisa letu ni MAISHA YA NDOA NA FAMILIA. Kwa roho ya kichungaji, tunapenda Kanisa la nyumbani liendelee kulishwa na kuimarishwa, kwa neno, sakramenti na mafundisho mbalimbali, ili kweli usitawi wake, uakisi usitawi wa Kanisa zima la Mungu.

Katika nyakati zetu hizi, ambapo Kanisa linapata changamoto nyingi kutokana na ubaridi wa watu katika kupokea na kutunza wito wa ndoa; na kwa upande mwingine changamoto ya mambo mbalimbali yanayoharibu uzito na unadhifu wa Kanisa la nyumbani; tunaungana na Baba Mtakatifu kuwaalika watu wote “MSIOGOPE KUJENGA FAMILIA”. Watu wengi kwa sababu ya uwoga, na pengine ubinafsi na uchoyo, hawapendi kujenga familia. Hawapendi kuzaa watoto kwa kisingizio cha gharama, au hakuna muda wa kuwatunza. Au wengine wataona watoto ni mzigo na karaha.

Tukiacha wajibu huo tuliopewa na Mungu, Kanisa letu tutamwachia nani? Sote tuone kwamba TUNAWAJIBU WA KULIJENGA KANISA LA SASA LA LA KESHO. Tunashiriki katika kulijenga Kanisa la kesho kwa kuwaandaa watu wema, wenye kumjua na kumpenda Muumba wao na hivyo kumtumikia kwa njia ya Kanisa lenye msingi katika familia bora.

Kipindi kijacho tutaendelea kwa kutafakari juu ya maandalizi ya kuupokea wito wa ndoa. Kwa vile ndoa ni wito, anayeupokea anapaswa kujiandaa vizuri kisaikolojia, kiroho na kijamii, ili tangu mwanzo ajue kwamba anapokea wajibu mkubwa na wa maana sana. Tunafanya hivyo ili, isitokee kwamba mtu anaangukia mahali ambaposio wito wake. Mtu anayeishi wito usio wa kwake, atateseka na kutesa wengine; na hatimaye atakosa mastahili.

TUSIWE PEKE YETU, TUMHUSISHE MUNGU KATIKA WITO NA MAISHA YA NDOA. Tunaendelea kuwaombea wote ambao tayari wapo katika maisha ya ndoa na familia, Mungu mwenyewe aliyewajalia wito huo, kwa msaada wa neema zake awasaidie kuuishi vema, ili yeye mwenyewe atukuzwe na wanadamu tuokolewe. BIKIRA MARIA MALKIA WA FAMILIA – UTUOMBEE.
Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.