2013-11-30 08:39:13

Vipaumbele vya AMECEA kwa Mwaka 2014- 2016: Familia, Vijana na Majadiliano ya kidini


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni katika mikakati yake ya kichungaji kwa Mwaka 2014 - 2016 limeamua kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: familia, vijana na majadiliano ya kidini, ili kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia; kutoa matumaini kwa vijana ambao ni jeuri ya Kanisa na kukoleza misingi ya haki na amani kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya.

Familia inapewa kipaumbele cha kwanza kwa kuzingatiwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameitisha Sinodi Maalum ya Maaskofu ili kujadili na kufanya tafakari ya kina kuhusu: fursa, changamoto na kinzani zinazojitokeza katika maisha ya ndoa na familia kwenye ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia mintarafu dhamana ya Uinjilishaji.

Nchi za AMECEA zinapenda kutoa matumaini kwa vijana kwa kukazia mikakati ya kichungaji kwa vijana kwa kukazia Utume wa Biblia na malezi ya vijana kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ili vijana waweze kulifahamu na kuliishi Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya ujana. AMECEA inaandaa mpango mkakati utakaotumiwa na Nchi wanachama.

AMECEA katika mikakati yake ya kichungaji kwa kipindi cha miaka miwili, inapenda kukazia umuhimu wa majadiliano ya kidini ili kujenga na kuimarisha haki, amani na utulivu, kwa kuzingatia kwamba, Jamii ya leo ni mkusanyiko wa watu wenye dini na imani mbali mbali, wanaopaswa kuheshimiana, kupendana na kusaidiana kwa hali na mali katika hija ya maisha yao hapa duniani. AMECEA inapenda kuwaelimisha waamini wake ili waweze kufahamu pia imani za dini nyingine ili kuheshimiana na kuthaminiana hata katika utofauti.

Wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inaposhuhudia athari za mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo mbali mbali ya Afrika, AMECEA inasema kwamba, kuna haja kwa Kanisa kuendelea kuhimiza utunzaji bora wa mazingira pamoja na ushiriki mkamilifu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.







All the contents on this site are copyrighted ©.