Majaribio ya kwanza ya chanjo ya Ukimwi kwa watoto wenye virusi vya Ukimwi yaonesha
mafanikio!
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka tarehe Mosi, Desemba, inaadhimisha Siku ya Ukimwi
Duniani. Kwa mwaka huu, Siku hii inapambwa na matumaini ya kupatikana kwa chanjo ya
watoto wenye virusi vya Ukimwi, iliyofanyiwa majaribio kwa watoto kumi katika Hospitali
ya Bambino Gesu, inayoendeshwa na kumilikiwa na Vatican.
Taarifa kutoka Hospitali
ya Bambino Gesu inasema kwamba, majaribio haya yamefanywa kwa kipindi cha miaka miwili
kwa watoto waliokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na matokeo yake kuchapishwa
kwenye Jarida la "Plos One", ili kutoa mwanya kwa mabingwa na wataalam wa afya kuweza
kuangalia mafanikio haya. Majaribio haya yamefanywa kwa watoto ambao walikuwa wameambukizwa
Ukwimwi tangu walipozaliwa na Mama zao.
Upatikanaji wa chanjo hii ni hatua
muhimu sana katika mchakato wa kupunguza matumizi ya dawa za kurefusha maisha zinazotolewa
kwa watoto walioathirika na ugonjwa wa Ukimwi. Taarifa inaonesha kwamba, chanjo hii
ni mchanginyiko wa dawa kadhaa zinazodhibiti ongezeko la Virusi vya Ukimwi na hivyo
kuuwezesha mwili kujijenga kinga yake. Pamoja na mafanikio hayo dawa hii bado inaonekana
kuwa na madhara kwa watoto kuwa na kikohozi cha muda mrefu.
Watoto wanaozaliwa
wakiwa wameambukizwa Virusi vya Ukimwi wanaweza kuanza kupata chanjo hii tangu mwaka
wao wa kwanza na wataendelea na dawa hizi katika maisha yao yote! Dawa hii inaweza
kusaidia kupunguza gharama za ununuzi wa dawa za kurefusha maisha pamoja na miundo
mbinu inayohitajika kwa ajili ya tiba hii.