2013-11-30 11:52:57

Amani na usalama ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele na Serikali ya Kenya


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaitaka Serikali ya Kenya kuharakisha mchakato wa kusitisha vita kati ya makabila ya Turkana na Pokot, ili kuokoa maisha ya watu wanaouwawa kutokana na kinzani hizi za kikabila. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na maboresho ya huduma za kijamii kama vile barabara.

Ni mwaliko uliotolewa na Askofu Dominic Kimengich wa Jimbo Katoliki la Lodwar pamoja na Askofu Anthony Crowley kutoka Jimbo Katoliki la Kitale. Maaskofu wanasema, kuna haja kwa serikali kuhakikisha kwamba, inatoa ulinzi na usalama kwa raia wake sanjari na maboresho huduma msingi za kijamii.

Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anasema, Serikali iwekeze zaidi katika mikakati ya ulinzi na usalama kwa kuvipatia vikosi vyake nyenzo za kufanyia kazi kwa uhakika. Anasema, kinzani za kikabila kati ya Jamii ya wafugaji na wakulima zinasababishwa na ugomvi wa malisho, maji, wizi wa mifugo pamoja na kugundulika kwa madini katika maeneo haya.

Wakati huo huo Baraza la Makanisa Kenya limeitaka pia Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kujizatiti katika masuala ya ulinzi na usalama, ili kuokoa maisha ya watu na mali zao. Mikakati hii inapaswa kwenda sanjari na elimu itakayowasaidia wananchi kutambua umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani. Wananchi wawajibike kudumisha amani na utulivu nchini Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.