Tanzania inaendelea kuwekeza kwenye miundo mbinu ya barabara kwa kasi kubwa!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameiongezea Tume ya
Mabadiliko ya Katiba siku 14 zaidi kuanzia Desemba 16, mwaka huu, 2013, ili kuiwezesha
kukamilisha kazi yake. Rais Kikwete ameiongeza Tume hiyo muda zaidi kufuatia maombi
ya Tume yenyewe na kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ameongeza muda wa Tume hiyo kufanya kazi kuanzia Desemba 16 hadi Desemba
30, 2013.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuiongezea Tume hiyo muda wa
kufanya kazi yake. Kufuatia maombi ya kwanza, Rais Kikwete aliiongezea Tume hiyo muda
wa siku 45 kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu, 2013. Chini ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, Tume hiyo inatakiwa kufanya kazi kwa miezi 18. Aidha, sheria
hiyo inampa Rais mamlaka ya kuiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi usiozidi siku
60.
Kwa uamuzi wake wa kuiongezea Tume hiyo siku nyingine 14, Rais Kikwete
atakuwa ameiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi wa jumla ya siku 59 kati ya 60
ambazo anaruhusiwa kisheria kuiongezea Tume hiyo.
Wakati huo huo, Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itaongeza kwa kiasi kikubwa kasi
ya kusambaza huduma za umeme na maji katika vijiji nchini kwa nia ya kuboresha maisha
ya wananchi. Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi wakati alipozindua
miradi ya maendeleo, Jumatano, Novemba 27, 2013, katika siku ya kwanza ya ziara ya
kikazi ya siku tano ambayo ameianza katika Mkoa mpya wa Simiyu.
Rais Kikwete
ameanza ziara hiyo kwa kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Bariadi-Lamadi
kwa kiwango cha lami katika sherehe iliyofanyika katika eneo la Old Maswa katika Wilaya
ya Bariadi. Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 71.8 itauunganisha Mkoa wa Simiyu
na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na inajengwa na Kampuni ya China Communication
Construction ya China kwa gharama ya Sh. Bilioni 67.4, fedha ambazo zinatolewa na
Serikali ya Tanzania ambayo tayari imemlipa mkandarasi huyo Sh.Bilioni 21.69.
Barabara
hiyo ambayo itakamilika katika miezi 30 ijayo, itakuwa na vituo 24 vya mabasi na ilifanyiwa
upembuzi wa kina kwa gharama ya Sh.milioni 710.
Akizungumza kwenye sherehe
ya uwekaji jiwe hilo la msingi, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake inatumia fedha
nyingi kujenga barabara nchini kwa sababu kama “tunadhani tunaweza kuendelea bila
kuunganisha nchi yetu kwa barabara za uhakika na kurahisisha usafiri na usafirishaji,
tunajidanganya.” Amesema kuwa barabara hizo zilitakiwa kujengwa miaka mingi iliyopita,
lakini nchi ilichelewa sana kuifanya kazi hiyo.
“Hizi barabara tulitakiwa kuzijenga
siku nyingi, lakini hali haikuruhusu. Chukua mfano wa ujenzi wa madaraja makubwa.
Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 1969 ulisema kuwa tungejenga madaraja yote makubwa kwenye
mito yetu mikubwa yote nchini, yaani Daraja la Kirumi kwenye Mto Mara, Daraja la Kilombero
kwenye Mto Kilombero, Daraja la Malagarasi kwenye Mto Malagarasi, Daraja la Kigamboni
la Dar es Salaam na Daraja la Rufiji kwenye Mto Rufiji,” amesema Rais na kuongeza:
“Lakini
Serikali ya Awamu ya Kwanza ilifanikiwa kujenga daraja moja tu la Kirumi…Mzee Mkapa
akajenga Daraja la Rufiji…na sisi tunajenga madaraja matatu – Kigamboni, Kilombero
na Malagarasi, ambalo limemalizika sasa. Sasa tusipojenga barabara wakati huu tutalazimika
kuzijenga baadaye tena kwa gharama kubwa zaidi na bila barabara nzuri na za uhakika,
uchumi hauwezi kupanuka kwa kasi inayostahili.”
Akizindua mradi wa usambazaji
umeme vijijini katika Parokia ya Nkololo katika Wilaya ya Bariadi, Rais Kikwete amesema
kuwa katika kusambaza huduma za umeme kwa kasi zaidi, Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini
(REA), utasambaza umeme katika vijiji 1,600 katika awamu ya kwanza ya kazi hiyo katika
muda mfupi.
Rais amesema kuwa usambazaji huo wa umeme wa REA ni tofauti na
usambazaji umeme unaofanyika chini ya Miradi ya Shirika la Maendeleo ya Milenia la
Marekani na Mradi wa Electricity Five unaogharimiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB). Chini ya miradi hiyo, vijiji 155 katika Mkoa wa Simiyu peke yake vitasambaziwa
umeme, kasi ambayo ilikuwa haijawahi kufikiwa wakati wowote katika historia ya Tanzania.
Kuhusu
maji, Rais Kikwete amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, Serikali yake
inatarajia kusambaza huduma ya maji katika vijiji 1,449 katika hatua inayokadiriwa
kuwa itawanufaisha watu wapatao milioni saba. Rais Kikwete anaendelea na ziara yake
katika Mkoa wa Simiyu kwa kutembelea wilaya za Itilima na Meatu. Mkoa wa Simiyu ni
moja ya mikoa minne ambayo iliundwa na Rais Kikwete mwaka 2012 na ina wilaya tano
ambazo ni Busega, Bariadi, Maswa, Meatu na Itilima.