Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio
Ni mara nyingine tena mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, kipindi tafakari masomo
Dominika. Kwa hakika Neno tunalolitafakari si Neno la kawaida bali ni Kristu mwenyewe
mkate wa uzima wa mbinguni. Ni mkate utupao
uzima. Tunapenda kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kumaliza mwaka wa Kanisa na sasa
Dominika hii tunaanza mwaka mpya wa Kanisa, yaani mwaka A Dominika ya kwanza ya Kipindi
cha Majilio. Mpendwa msikilizaji, katika kipindi cha Majilio, Mama Kanisa daima
apenda kutukumbusha ujio wa Bwana Masiha, kwamba Bwana hakuja mara moja tu, bali anakuja
kwetu siku zote, wakati wa raha na taabu. Ndiyo kusema yuko katikati yetu, yuko katika
Kanisa, yuko kati ya wale wanaotangaza Injili na kuishi maisha ya upatanisho na amani.
Masiha anapokuja mara zote na kukaa nasi anatudai mabadiliko ya ndani yaani maisha
yetu, tunaitwa kuendana na ujio wake. Tunaitwa kubadili tabia zetu na mienendo yetu.
Ndiyo kusema tunaalikwa kutayarisha njia ya Bwana, kutayarisha kuzaliwa kwa Masiha.
Hali hii daima yatupa furaha inayotusaidia kujiandaa kwa ajili ya ujio wa pili ambapo
Bwana Masiha wetu atakuja kama Hakimu mwenye haki na si kama Mtoto Emanueli. Mpendwa
mwana wa Mungu, tunaalikwa na tunapaswa kuwa tayari kwa ajili ya ujio kama ambavyo
masomo ya Dominika hii ya I ya Majilio yanavyotufundisha. Tunapata kutafakari masomo
yetu ya Dominika hii tukiongozwa na kauri mbiu ya Kesheni na kusali maana hamjui siku
wala saa atakayokuja Mwana wa mtu. Mwana huyu wa mtu anakuja kuanzisha dunia mpya,
na Yerusalemu kutakuwa kitovu cha ulimwengu. Kumbe, ujio wa Masiha ni ujio wa
nuru, ni kuwaweka watu pamoja wakiielekea Yerusalemu mpya ya mbinguni. Injili ya Matayo
ndiyo Injili ambayo itaongoza kipindi hiki cha Majilio na mwaliko utakuwa ni kukesha
na kusali, kutenda matendo ya huruma na mapendo na kushika vema maagano yetu katika
hali ya kila mmoja wetu. Mpendwa msikilizaji, sehemu ya Injili ya Dominika hii
yaani kutoka katika, Mt. 24:37-44 inasimikwa katika sura hiyohiyo ya 24 aya za kwanza,
ambapo wanafunzi wanamwonesha Masiha, majengo na mahekalu mbalimbali, wakifikiri ni
ya maana sana kwake , na Masiha atawaambia haya yote ni ubatili mtupu na yatabomolewa
na hakuna kitakachosalia! Habari na maneno haya ni ya kieskatolojia, yaani yazungumza
habari za mwisho wa maisha yetu hapa duniani. Masiha akisha kuwaambia hilo baadaye
atakuwa katika mlima wa mizeituni na hapo tena wanafunzi wake watamwuliza faraghani
wakisema haya yatatukia lini? Basi Bwana ambaye hafuati vionjo, bali hufundisha kilicho
cha kweli, atatoa jibu tofauti na udadisi wao, ndiyo kusema jibu ambalo latufaa sisi
hivi leo na kwa wakati ujao. Anawapa jibu akitoa mfano wa gharika kuu la Noa na mwisho
atasema, BASI KESHENI KWA MAANA HAMJUI SIKU WALA SAA. Mpendwa msikilizaji, je jambo
lililowapata watu wakati wa Noa laweza kutokea hivi leo? Natumai yawezekana! Ndiyo
kusema, tukijaribu kufanya utafiti katika Neno la Mungu, tunaona Bwana akisema, maana
nyakati hizo wakati kabla ya gharika watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa
na mpaka Noa anaingia katika safina hawakuwa na habari isipokuwa wachache. Mambo
ya ulevi, kuoa kusikokuwa katika mpango wa Kimungu, kutumbua na kula pasipo kuwajali
maskini ni mambo ya kila siku katika jamii zetu, na hivi gharika la Nuhu kwa namna
tofauti linakuja kila siku! Hatuko mbali nalo! Angalia vifo vya watoto na watu
wazima kwa sababu ya kukosa matibabu na zaidi sana uaminifu. Angalia uwepo wa watoto
ambao tunawaita “watoto wa mitaani”, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi,
angalia ugomvi, vita na machafuko ya kidini na madhulumu mbalimbali. Haya yote ni
magharika ambayo yanapelekea jamii na maisha yetu kuporomoka. Mpendwa mwana wa
Mungu, bado tunayo nafasi ya kupambana kinyume na magharika haya, na kwa hakika ni
kujitwalia siraha za mwanga, nikujikabidhi mikononi mwa Masiha anayekuja kuleta amani
na utulivu katikati yetu. Kumbe ujumbe wa Neno la Mungu katika Dominika hii kama tulivyokwishasema
yaani Kesheni kila siku na kusali kwa maana hamjui siku wala saa ni wa kweli kwa wakati
wetu. Kukesha katika maandalizi ni ile hali ya kujikabidhi mikononi mwa Mungu
tangu Dominika ya I ya Majilio mpaka Sherehe ya Yesu Kristu Mfalme. Ni kuweka daima
mbele, masilahi ya jumuiya zaidi ya masilahi yangu binafsi. Bwana akisonga mbele katika
mafundisho yake katika Dominika hii anaweka tena mfano mwingine kuhusu siku ya mwisho
akisisitiza maandalizi ya dhati, akisema, wanawake wawili watakuwa wanasaga na mmoja
atatwaliwa na mwingine ataachwa! Bwana ataka kusema kuwa hata katika maisha ya kawaida
ya kila siku ni lazima kukesha. Ndiyo kusema tukiwa barabarani tukeshe, tukiwa kondeni
tuziimbe sifa za Bwana na kuzitaraji daima fadhili za Bwana. Mpendwa msikilizaji,
usikubali kupoteza muda hata kidogo, daima ishi kwa kugawa na kuwashirikisha mapendo
ya Mungu watu wote. Nikienda kuangalia historia ya Mtakatifu Gaspari mwanzilishi wa
Shirika la Wamissionari wa Damu Takatifu, katika maisha yake alijitahidi kuipanua
siku yake yaingie mawazo na matendo yake yote mema. Huu ni mwujiza, yaani siku ya
masaa ya 24 inapanuliwa kwa ajili ya mapendo, na huko ndiko kuishi utayari wa kumpokea
Masiha. Mtakatifu Gaspari alifuata nadharia ya “Elasticity ya mapendo”! Mpendwa
msikilizaji, tunarudia kwa ajili ya kukaza mafundisho, hivi kukesha kwaweza kuwa na
maana gani tena? Ni kuhakikisha nafasi zote alizotupa Mwenyezi Mungu, tunazitumia
vema. Nafasi zenyewe ni kutunza maisha ya sala, kuwajibika katika kazi, katika ndoa,
katika upadre na maisha ya kitawa. Bwana wetu Yesu Kristu yuko daima katika nafasi
hizo akitaka kutujaza furaha kamilifu. Kazi kubwa kumbe ni kuwa macho kuona ujio wake
katika maisha hayo. Mpendwa msikilizaji Mt Paulo anatupa tumaini akisema, wokovu
wetu unakaribia na usiku unakwisha na mchana unaingia, tutupilie yote yatuleteayo
aibu, tujitwalie siraha za mwanga. Anasisitiza kurudi katika ubatizo wetu na kutenda
kadiri ya ubatizo, kuachana na matendo ya kipagani, yaani ulafi, ujeuri, rushwa, ufisadi
wa mali ya umma na mambo kama hayo. Mpendwa msikilizaji, ninapenda kukukumbusha
kuwa mkristo ni mtu mwenye kuzitarajia siku za usoni kwa furaha, kwa sababu lengo
la maisha yake siyo kuishi hapa duniani, bali ni kuufikia uhai usioharibika, yaani
uzima wa milele. Mkristo anaishi hapa duniani akijiweka tayari kukutana na Bwana wake
ambaye siku ile ya mwisho atamwalika aingie katika raha ya milele na kuishi naye daima.
Kumbuka kuwa tukio la kurudi ghafla kwa Masiha halimtishi mtu, ingawa hofu kidogo
yapaswa kuwepo! Kwa nini halitishi, ni kwa sababu mtu akiwa tayari katika maisha yake
basi siku ya mwisho ni kumalizia matayarisho yake ambayo yako tayari! Huyu anayejiweka
tayari siku zote anayohamu daima akisubiri siku hiyo kwa furaha. Basi mpendwa
tupilia mbali vinyago ulivyonavyo na matunguli ya kiroho ili ukae mkao wa kumpokea
Mwumba wako anapokuja kila siku na siku ya mwisho.
Ninakutakia majilio njema
na mwanzo wa mwaka wa Kanisa wa furaha. Tumsifu Yesu Kristo na Bikira Maria.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.