Marehemu Askofu John Andrea Simalenga azikwa kwa heshima kubwa mjini Njombe!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameongoza mamia ya watu kwenye ibada ya mazishi
ya Askofu wa Saba wa Dayosisi ya South West Tanganyika ya Kanisa la Anglikana Tanzania
Mhashamu Askofu John Andrea Simalenga iliyofanyika Njombe mjini. Akizungumza
na mamia ya waumini na waombolezaji waliohudhuria ibada hiyo ya mazishi Alhamisi,
Novemba 28, 2013 Waziri Mkuu alisema Dayosisi hiyo imepoteza mhimili muhimu lakini
akawataka wawe na umoja na upendo huku wakiendelea kumtumainia Mungu.
“Mhashamu
Baba Askofu Simalenga alisimikwa Julai 6, 2008. Ni miaka mitano tu ya utumishi
kwenu na alikuja wakati ambapo Dayosisi hi ilikuwa imekaa kwa miaka 10 bila ya kuwa
na kiongozi. Siku anawekwa wakfu nilikuwepo na ninakumbuka mlimuomba asaidie kuleta
mshikamano,” alisema Waziri Mkuu. “Ninawaomba wanadayosisi muwe na upendo na mshikamano
mkubwa miongoni mwenu hadi hapo Mungu atakapotupatia kiongozi mwingine. Tumuombe Mungu
ili kiongozi huyu ajaye apatikane kwa njia ya amani,” alisisitiza.
Alimwomba
mke wa marehemu, Bibi Martha pamoja na watoto wa marehemu waupokee msiba huo kwa
mikono miwili na kuahidi kuwaombea faraja kwa Mwenyezi Mungu. Waziri Mkuu ambaye
alishiriki mazishi hayo kwa niaba ya Serikali, Alitumia fursa hiyo kuwapa pole maaskofu,
mapadre, watawa na familia zikiwa ni salamu maalum kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete
ambaye alisema yuko ziarani kwenye mkoa mpya wa Simiyu.
Naye Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bibi Anne Makinda ambaye pia ni mbunge wa Njombe
Kusini ilipo Dayosisi hiyo akitoa salamu za rambirambi alisema wana Njombe wamepungukiwa
na nguvu kwa kuondokewa na Askofu Simalenga. “Alisaidia kuleta umoja hapa kwetu, tumempoteza
mtu muhimu sana katika harakati za maendeleo ya wilaya yetu na mkoa kwa ujumla. Alisaidia
kuleta umoja na upendo na sisi tuwe na upendo na amani, tuendelee kumuomba Mungu hadi
tutakapoletewa msimamizi mwingine. Katika mahubiri yake kwenye ibada hiyo, Askofu
Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mhashamu Jacob Chimeledya aliwataka waumini
wote wamtazame Mungu na wamtegemee Mungu kwa sababu wanampenda lakini yeye ameona
ni vema ampunzishe mtumishi wake. “Sote tunajua kuwa katika kipindi chake, Dayosisi
hii ilitulia kabisa Je, tutaruhusu kuondoka anikwake kuzue tena chokochoko? Msiba
huu usifike mahali ukaanza kututenganisha na kutoa mwanya wa kuanza kunyoosheana vidole.
Tumuombe Mungu atusaidie afute machozi yetu,” alisema.
Askofu John Andrea Simalenga
alizaliwa Novemba 30, 1953 na kufariki Novemba 24, 2013 baada ya kuugua kwa siku
mbili. Novemba 22, 2013 alijisikia vibaya na alipopimwa aliikutwa na malaria, kisukari
na shinikizo la damu. Alilazwa hospitali ya Kibena, Njombe na kuruhusiwa siku iliyofuata
lakini Novemba 24 alizidiwa tena na kuaga dunia. Ameacha mjane na watoto wanne.