2013-11-29 07:37:25

Kijiji cha Matumaini ni kielelezo cha Injili ya Furaha na Matumaini kwa watoto walioathirika kwa virusi vya Ukimwi


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, Injili ya Furaha, anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kumwiga Kristo aliyejifananisha na watu wadogo wanaohitaji msaada, jambo ambalo ni changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi unaoelemewa zaidi na ubinafsi na hali ya mtu kujitegemea, kiasi hata cha kushindwa kuwekeza katika mchakato wa kuwasaidia wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni Jamii kuonja fursa mbali mbali zinazotolewa katika maisha.

Kijiji cha Matumaini kinachomilikiwa na kuendeshwa na Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu kwa ajili ya watoto yatima na walioathirika na ugonjwa wa Ukimwi, kilianzishwa kunako mwaka 2002 katika harakati za kusaidia kuwajengea matumaini watoto waliokuwa wameathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi. Padre Vincent Boselli muasisi wa Kijiji cha Matumaini katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha kwamba, Kijiji cha Matumaini kimepiga hatua kubwa katika kuwasaidia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, Kanda ya Kati nchini Tanzania.

Katika mikakati yao kwa watoto walioathirika na Ukimwi, walianza kuwapatia dawa za kurefusha maisha na kwamba, watoto watatu wa kwanza kabisa hadi leo hii bado wako hai na wanaendelea na masomo ya shule ya Sekondari.

Kijiji cha Matumaini kimeanzisha na kuendesha kampeni ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa na kunyonyesha na kuna mafanikio makubwa, kwani idadi ya watoto wanaozaliwa pasi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi wameongezeka maradufu kwenye Kijiji cha Matumaini.

Hadi sasa wanawasaidia watoto wenye Virusi vya Ukimwi ambao si yatima na wanaendelea kutunzwa na wazazi wao. Watoto hawa wanapewa huduma nje ya Kijiji cha Matumaini na kwamba, kuna idadi kubwa ya watu walioathirika na Virusi vya Ukimwi wangependa kupata huduma kutoka kwenye Kijiji cha Matumaini, lakini Padre Vincent anasema, inashindikana kuweza kuwahudumia watu wote hawa ingawa pia ni vigumu kuwashauri kwenda kupata huduma sehemu nyingine.

Kwa hakika, Kijiji cha Matumaini ni kielelezo cha Injili ya Furaha na Matumaini kwa watoto walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi, Kanda ya Kati, nchini Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.