Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF katika taarifa yake iliyozinduliwa
tarehe 29 Novemba 2013 inaonesha kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mchakato
wa kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto tangu
mwaka 2005 hadi mwaka 2012. Watoto 850, 000 wamekingwa dhidi ya maambukizi ya virusi
vya Ukimwi, lakini hali inatisha miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.
Maambukizi
kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto yamepungua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha Mwaka
2009 hadi mwaka 2012: Ghana kwa 76%, Namibia 58%, Zimbabwe 55%, Malawi 52%, Botswana
52%, Zambia na Ethiopia ni 50%. Wanawake walioathirika kwa virusi vya Ukimwi kwa asilimia
60 kutoka katika nchi zinazoendelea wamepata huduma ya afya ili kudhibiti maambukizi
ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto.
Kwa mwaka 2012 ni watoto
34% tu waliobahatika kupata dawa za kurefusha maisha, ikilinganishwa na asilimia 63%
ya watu wazima. Inakadiriwa kwamba, katika kipindi hiki watoto 210,000 wamefariki
kutokana na Ukimwi pamoja na magonjwa mengine nyemelezi. Kuna watoto ambao wanaishi
na virusi vya Ukimwi bila kupata tiba na wanatarajiwa kufariki dunia katika kipindi
cha miaka miwili, ikiwa kama juhhudi za makusudi hazitafanyika kuwapatia dawa za kurefusha
maisha.