2013-11-28 11:02:35

Hakuna Ukristo wa kweli pasi ya kulifahamu Fumbo la Pasaka!


Tarehe 16 Novemba 2013 ni siku iliyoingia katika historia ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Loyola, umati wa waamini wa Jimbo Kuu walikusanyika katika kuadhimisha kilele cha Mwaka wa Imani.

Ibada ya kilele ilitanguliwa na maandamano yaliyojaa shamrashamra ya waamini wengi wao wakiwa wameshika matawi ya miti toka dekania zote saba za Jimbo. Maandamano haya ya kila dekania yaliingia katika viwanja vya Loyola wakiwa wamebeba zana walizokabidhiwa kila dekania siku ya kufungua Mwaka wa Imani. Zana hizi za kiimaani ni Msalaba wa Mwaka wa Imani, Bango la Mwaka wa Imani na Bendera ya Mwaka wa Imani. Zana hili zilizungushwa katika kila parokia, vigango, jumuiya na kila familia.

Ibada ya Misa ya kilele cha Mwaka wa Imani iliongozwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akisaidiwa na maaskofu wasaidizi Eusebius Nzigilwa na Titus Mdoe, pamoja na wakreli mia na siti na moja. Katika homilia yake Mwadhama alisisitiza juu ya nafasi ya pekee ya Msalaba katika kuishi imani ya kweli ya kikristo. “Bila Msalaba, hakuna imani ya kikristo” alisisitiza Mwadhama.

Katika Misa hii ya kilele watoto mia arobaini walibatizwa, wakiwakilisha watoto elfu kumi waliobatizwa katika kipindi chote cha Mwaka wa imani. Mwisho wa ibada hii Mwadhama alitoa baraka ya rehema kamili kwa waamini wote waliokuwa wamejiandaa kupokea rehema kamili.

Katika adhimisho hili, kama ishara ya kuipokea kwa mikono miwili Katekesimu ya Kanisa Katoliki katika maisha ya kila siku ya kichungaji ya Jimbo. Mwadhama Polycarp Karidnali Pengo alizindua Katekesi ya Kanisa Katoliki iliyoandaliwa kwa kuwashirikisha makatekista kwa ajili ya watoto walioko katika mafundisho ya Komunyo ya Kwanza.

Tukio la pekee katika ibada hii, ni mvua kubwa iliyonyesha katikati ya ibada. Licha ya ukubwa wa mvua na sehemu kadhaa za uwanja kujaa maji, waamini walibaki watulivu na kushiriki kikamilifu ibada mpaka mwisho. Jambo hili lilimfariji kwa namna ya pekee Mwadhama na kuwashukuru waamini wote ambao walionesha ukomavu wao, licha ya mvua hiyo.

Mwadhama Pengo, aliwaasa waamini katika salamu zake, mwisho wa Misa hiyo kuwa kufunga Mwaka wa Imani, si ndio mwisho wa imani, bali sasa kila mwamini anapaswa kuendelea kuishi imani yake kwa namna bora zaidi, akiutazama Msalaba wa Kristo kama dira ya maisha yake ya kila siku.








All the contents on this site are copyrighted ©.