2013-11-27 09:58:36

Wakapuchini wanaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu walipofika Jimboni Dodoma


Kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Imani Jimbo Katoliki Dodoma, kimekwenda sanjari na sherehe za Jubilee ya Miaka 50 tangu Wamissionari ndugu Wafrancisko Wakapuchini kutoka Toscana, Italia walipowasili Jimbo Katoliki la Dodoma na kukabidhiwa Parokia za Kibakwe na Mpwapwa. Wamissionari hawa wameendelea kuwa ni chachu ya maendeleo ya wananchi wa Dodoma kiroho na kimwili, kwa kuwashirikisha ile furaha ya Injili ya Kristo.

Katika Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Dhahabu kwa Wamissionari Ndugu Wafrancisko Wakapuchini, Vikarieti ya Mpwapwa Jimbo Katoliki la Dodoma, Askofu Gervas Nyaisonga amewashukuru Wamissionari hao kwa niaba ya Jimbo Katoliki la Dodoma. Kurejea kwao tena mahali ambapo walifanya kazi kwa miaka 50 ni kuonesha moyo wa rehema, utu wema, upole, uvumilivu, unyenyekevu, huku wakijivika upendo kwa Mungu na jirani. Haya ni mambo msingi yanayoweza kumfanya mtu kurejea tena kwenye miliki yake ya zamani.

Jubilee iwe ni fursa makini ya kurudia tena ahadi ya kujikita katika Ujinjilishaji mpya, kwa kukazia upendo na mshikamano; toba na wongofu wa ndani; kwa kufundishana na kuonyana kidugu; daima wasaidiane kuchichumilia utakatifu wa maisha wakiongozwa na Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Sheria na Kanuni za Shirika; kwa kujitahidi kumwilisha mashauri ya Kiinjili katika maisha na utume wao kama Wamissionari.

Askofu Nyaisonga amewataka Wamissionari hawa kubadilika bila ya kukata tamaa na kwamba, toba, wongofu wa ndani na mabadiliko ni sehemu ya cheche za furaha kwa waamini wa Jimbo Katoliki la Dodoma, wakati huu Mama Kanisa anapojikita zaidi na zaidi katika Uinjilishaji Mpya kama njia ya kurithisha imani ya Kikristo ili kukabiliana na changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Ndugu Wafranciskani Wakapuchini walifika nchini Tanzania na kuelekea Jimboni Dodoma kunako Mwaka 1963, wakakabidhiwa Parokia ya Kibakwe na Mpwapwa. Leo hii Wakapuchini wameenea katika Majimbo mbali mbali nchini Tanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.