KAICIID yaanzisha ushirikiano na mashirika ya kimataifa ili kukoleza ari na moyo wa
ushirikiano na majadiliano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali!
Kituo cha Majadiliano ya Kidini na Kitamaduni cha Mfalme Abdullah Bin Aziz, kwa kifupi
KAICIID, kilichohitimisha warsha ya siku mbili huko Vienna, Austria kinasema kwamba,
kimeanzisha ushirikiano wa pekee na Mashirika ya Kimataifa na kwamba, kati ya Mashirika
haya ni: Umoja wa Afrika; Taasisi ya Elimu ya Dini ya Kiislam, Shirika la Kimataifa
la Sayansi na Utamaduni, Mfuko wa Skauti Kimataifa pamoja na Shirika la elimu, sayansi
na utamaduni la Umoja wa Mataifa.
Kituo hiki kinapania pamoja na mambo mengine
kuendeleza mchakato wa elimu na majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini
mbali mbali duniani ili kujenga mazingira ya amani, utulivu na maendeleo endelevu.
Elimu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipambele
cha kwanza ili kujenga mahusiano thabiti ndani ya Jamii na kuepusha misimamo mikali
ya kidini na kiimani, ambayo imekuwa ikisababisha majanga sehemu mbali mbali za dunia.
Kituo
hiki kimekuwa ni chombo ambacho kinawaunganisha wasomi, watunga sera, viongozi wa
kidini na wapenda amani ili kwa pamoja kuweza kujadili mambo msingi na tete yanayomzunguka
mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni
matumaini ya viongozi wa kituo hiki cha majadiliano ya kidini kwamba, utekelezaji
wa mikakati hii utaanza kufanyiwa kazi ili kujenga na kuimarisha ushirikiano na majadiliano
na wadau mbali mbali.