2013-11-27 08:27:57

Chuo Kikuu cha Kikatoliki Kusini mwa Sudan ni bandari ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya!


Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan hivi karibuni, liliweka Jiwe la Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Kusini mwa Sudan, katika Ibada iliyooongozwa na Askofu Barani Eduardo Hiiboro wa Jimbo Katoliki la Tombura- Yambio, Kusini mwa Sudan. Katika hotuba yake, aliwataka wanafunzi watakaopata fursa ya kuchota ujuzi na maarifa, elimu na hekima kuhakikisha kwamba, wanagundua utajiri mkubwa unaofumbatwa katika tofauti za kitamaduni, kikabila na kidini.
Kanisa linaipongeza Serikali kwa kuchangia kwa hali na mali katika kuhakikisha kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Kusini mwa Sudan kinaanza, huko Juba na kwamba, hili ni tukio la kihistoria litakalokumbukwa na wengi! Anakipongeza Kikosi kazi kwa kupanga na kutekeleza kwa umakini mkubwa dhamana hii; kwa kuwa na mwono mpana na ujasiri wa kutekeleza ndoto hii na kuwa ni jambo halisi katika historia ya wananchi wa Sudan ya Kusini.
Chuo Kikuu cha Kikatoliki Kusini mwa Sudan ni bandari ya matumaini kwa vijana wa kizazi kipya nchini humo; mahali pa kuwafunda viongozi wa kitaifa na kwamba, hiki ni Chuo kikuu cha kwanza kujengwa Sudan ya Kusini, miaka thelathini na miwili tangu wazo hili lilipobuniwa kwa mara ya kwanza na Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan.
Chuo kinapania kuchochea maendeleo endelevu kwa wanafunzi kutoka ndani nan je ya Sudan, kwa kutambua umuhimu wa elimu katika mchakato wa maendeleo ya binadamu; watu ambao watakuwa na ujuzi na ufahamu wa kujenga Sudan iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hizi ni cheche za matumaini na maarifa katika mapambano dhidi ya janga la ujinga na umaskini.
Hapa anasema Askofu Barani Eduardo Hiiboro, pawe ni mahali pa kutafuta ukweli na kuukumbatia; kwa kuongozwa na tafiti za kisayansi na kibinadamu ili kuleta maboresho makubwa katika maisha ya watu, hasa wale wanaoishi vijijini, ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea sekta ya kilimo ili kupata mahitaji yao msingi. Chuo kizingatie sheria, sera, kanuni na viwango vinavyotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wahadhili wajisikie kuwa ni vyombo vya huduma kwa ajili ya kurithisha ujuzi na maarifa miongoni mwa wanafunzi; daima wafarijike kuona ubora na maendeleo ya wanafunzi wao.
Elimu ni nyenzo muhimu sana katika kuwajengea watu uwezo wa kiuchumi katika kupambana na mazingira yao. Huu ni mchango wa sekta binafsi ambao sasa unaanza kuthaminiwa na Serikali na kwamba, wadau mbali mbali katika sekta ya elimu watachangia kwa hali na mali katika kuwekeza kwenye ubora wa elimu inayotolewa nchini Sudan ya Kusini na kwamba, wasomi kutoka Sudan watachangia ustawi na maendeleo ya watu wao.
Chuo kiwasajili wanafunzi wenye sifa na viwango vinavyohitajika: uwezo wa masomo darasani, tabia njema na utashi wa kutaka kusoma na kujiendeleza zaidi. Chuo kikuu cha Kikatoliki Sudan kinataka kujenga na kuimarisha vyama vya kiraia ili viweze kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Jamii.








All the contents on this site are copyrighted ©.