Serikali za mitaa zishirikiane na sekta binafsi kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya
watu!
Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema anatamani kuona Serikali za Mitaa hapa
nchini zinasimamia maendeleo kuanzia ngazi ya chini kwa kushirikiana na sekta binafsi
ikiwa ni njia ya kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Ametoa kauli hiyo huo
Jumatatu, Novemba 25, 2013 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kufungua mkutano wa ushirikiano baina ya Mamlaka za Serikali za Mitaa za China na
Tanzania ulioanza Jijini Dar es Salaam.
“Ni muhimu tukaanzisha ushirikiano
huu kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa kwa sababu usimamizi wake unakuwa karibu zaidi
na wananchi kuliko ilivyo hivi sasa”, alisema.
Kuhusu ujio wa magavana, mameya
na wafanyabiashara wapatao 71 kutoka majimbo manne ya Shandong, Liaoning, Shaanxi
na Jilin, Waziri Mkuu alisema ujio wao umekuja wakati muafaka kwani unasaidia kujenga
mahusiano ya karibu zaidi na wananchi kwenye ngazi ya chini kuliko inavyokuwa kuna
mahusiano kwenye ngazi ya Kitaifa peke yake.
“Hawa waliokuja wanatoka majimbo
manne tu kati ya majimbo 31 ya nchi hiyo, tungependa kila mwaka tupate wajumbe wa
aina tofauti hadi tufikishe majimbo 15 au 20 hivi... tunataka ushirikiano huu ukue
zaidi uende hadi katika miji mikubwa ya Beijing ama Shanghai,” aliongeza.
Katika
hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo, Waziri Mkuu aliwataka watumie fursa hiyo kubadilishana
uzoefu na kufanikisha mahusiano ya kibishara si tu baina yao, bali hata katika ngazi
ya Halmashauri wanazotoka baadhi ya wajumbe.
Mapema akizungumza na washiriki
wa mkutano huo, Balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Youqing alisema biashara kati
aya China na Tanzania imeongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.47 ambalo
ni ongezeko la asilimia 15.2 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka jana.
Alisema
hadi kufikia Juni, 2013, makampuni zaidi ya 500 kutoka China yalikuwa yamekwishasajiliwa
hapa nchini yakiwa na mtaji wa Dola za Marekani bilioni 2.175 na kuifanya China iwe
ni mwekezaji wa pili kwa ukubwa hapa nchini Tanzania.
Naye Naibu Gavana wa
Jimbo la Shandong, Bw. Xia Geng ambaye pia ni kiongozi wa msafara huo, alisema Agosti,
2013 China ilileta madaktari 23 wa fani tofauti ili kusaidia kujenga kada ya watalaam
wa sekta ya afya hapa nchini.
Alisema maeneo makuu ambayo wamelenga kuyazingatia
katika ziara yao hii ni Kilimo; Nishati; Utunzaji wa Mazingira na uchimbaji wa rasilmali
za ardhini.
Alisema ifikapo mwaka 2014, wakati Tanzania na China zinatarajiwa
kuadhimisha miaka 50 ya urafiki baina yao, angependa kuona maeneo hayo ya msingi yakiwa
yamepewa kipaumbele katika utekelezaji wake.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na
Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Asiyekuwa
na Wizara Maalum), Prof. Mark Mwandosya, Wakuu wa mikoa 25, Makatibu Tawala wa Mikoa
25, Wakuu wa Wilaya 50, Wakurugenzi wa Halmashauri 95 na wafanyabiashara kadhaa.