2013-11-25 07:25:18

Jubilee ya Miaka 50 ya uhuru wa Kenya kumekucha!


Kanisa Katoliki nchini Kenya imekuwa ni mdau wa maendeleo endelevu ya mwanadamu kiroho na kimwili katika sekta ya elimu, afya, mawasiliano na maendeleo endelevu ya mwanadamu katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema kwamba, liko tayari kuungana na wananchi wa Kenya katika kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, Kenya itakapokuwa inaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu ilipojipatia uhuru wa bendera kutoka kwa Mwingereza.
Hayo yamebaianishwa na Padre Vincent Wambugu, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya na kwamba, Kanisa daima limewasindikiza wananchi wa Kenya katika hija ya maisha yao ka takribani miaka hamsini na litaendelea kufanya hivyo, kuelekea katika maisha ya uzima wa milele.
Jubilee ya Miaka 50 ya uhuru wa Kenya iwe ni fursa ya kujiwekea mikakati makini ya kuwahudimia wananchi wa Kenya kwa ari na moyo mkuu kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limekwisha panga mikakati ya maendeleo kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia sasa na kwamba, huu utakuwa ni mchango muhimu sana katika kutafuta mafao ya wengi na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Kenya. Kanisa Katoliki Kenya linamiliki na kuendesha kiasi cha asilimia 30% ya taasisi zote za sekta ya afya nchini humo. Lina Hospitali 54, Vituo vya Afya 83 na Zahanati 311.
Kanisa lina miliki taasisi za elimu zipatazo 8000; kati ya hizi, kuna shule za msingi 5600, Sekondari 1900, Taasisi za elimu ya juu 5 na Chuo Kikuu kimoja. Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Kenya itafikia kilele chake kati ya tarehe 11 na 12 Desemba 2013 kwenye Bustan za Uhuru na Kiwanja cha Karasani. Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho haya.








All the contents on this site are copyrighted ©.