2013-11-24 15:12:11

Yesu Mfalme ni kiini cha kazi ya uumbaji, Watu wa Mungu na mshikamano wa kidugu!


Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu inayohitimisha Mwaka wa Kanisa, inafunga pia virago vya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI, ambaye Mama Kanisa anapenda kumshukuru na kumpongeza kwa mwono wake mpana kwa maisha na utume wa Kanisa.

Mwaka wa Imani imekuwa ni fursa makini kwa waamini kugundua tena umuhimu wa hija ya imani iliyoanzishwa kwa Sakramenti ya Ubatizo na hivyo kuwawezesha waamini kuwa ni watoto wa Kanisa, wanaotembea kuelekea kwenye lengo la maisha ambalo ni kukutana na Mwenyezi Mungu; wakitakaswa na kutakatifuzwa na Roho Mtakatifu, ili furaha ya kweli iweze kujikita katika sakafu ya mioyo yao!

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya kufunga rasmi Mwaka wa Imani, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, sherehe za Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Amewashukuru na kuwapongeza viongozi wakuu kutoka Makanisa ya Mashariki waliohudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu, kielelezo cha umoja na mshikamano wa imani na uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kulipa kwa gharama ya maisha yao!

Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee Wakristo wanaoishi Nchi Takatifu, Syria na Mashariki ya Kati, ili waweze kupata amani na utulivu. Anasema, Liturujia ya Neno la Mungu inamweka Kristo kuwa ni kiini cha kazi ya: uumbaji, historia na kati ya watu wake. Yeye ni Mwana mzaliwa kwa kwanza na utimilifu wa yote na kwamba kila kitu kitajipatanisha naye! Ni mwaliko kwa waamini kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai kwa mawazo, maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo yao adili. Kinyume cha hapa anasema Baba Mtakatifu ni uharibifu mkubwa mazingira na binadamu mwenyewe.

Kristo ni kiini cha Watu wa Mungu, hali inayonesha jinsi ambavyo mwanadamu anatafuta uwepo wa Mungu katika maisha yake. Huyu ni Mungu ambaye amejifanya jirani na binadamu, ili aweze kuwa ni mwenza na ndugu katika maisha yake. Kristo ni kielelezo cha mkusanyiko wa Watu wa Mungu, anayemhudumia mwanadamu kwa gharama ya maisha yake kama sehemu ya utambulisho wa wafuasi wake. Ni taa ya matumaini hata katika giza la maisha!

Baba Mtakatifu anasema, yule mwizi aliyemtambua Yesu kuwa ni Mfalme, anaonja chemchemi ya huruma na msamaha, kwani alionesha ujasiri wa kuomba msamaha kutoka kwa Kristo na matokeo yake anakirimiwa kile alichoomba kwa imani na ujasiri mkuu. Haya ni maneno yenye matumaini kwa wale wanaomba rehema na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na kwamba, wanakirimia hata na zaidi ya kile walichoomba. Yesu ni kiini cha matamanio ya furaha na wokovu.







All the contents on this site are copyrighted ©.