2013-11-24 08:01:09

Wakatekumeni wanaalikwa: kusikiliza kwa makini, kukutana na kutembea na Yesu katika hija ya maisha yao ya Imani!


Katika kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jumamosi jioni tarehe 23 Novemba, 2013, Baba Mtakatifu Francisko kwa furaha kuu aliwapokea waketekumeni 500 kutoka katika nchi 47 walioanza safari ya kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Anasema, Neno wa Mungu alifanyika mwili ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kwa njia ya Ubatizo, mwamini anakufa na kufufuka pamoja na Kristo tayari kuanza hija ya maisha mapya.

Wakatekumeni hao baada ya kumtafuta Mwenyezi Mungu, sasa wako tayari kuonja huruma na upendo wake katika maisha yao na kwamba, Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza Wakatekumeni kudumu katika nia njema ya kukutana na Mungu anayeishi ndani mwao, hadi pale watakapomwona uso kwa uso. Wakatekumeni wanataka kufanya hija ya mang'amuzi ya uwepo wa Mungu katika maisha yao. Kiu ya imani inapokauka na kupotea anasema Baba Mtakatifu imani inageuzwa kuwa ni jambo la mazoea na inaweza kuzimika kama moto wa "kibatari".

Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia. Wanafunzi wake walimtambua na kuwaonesha wengine ile furaha ya kukutana na kuishi pamoja na Yesu. Hija ya maisha ya Mkatekumeni yamegawanyika katika sehemu kuu tatu: kusikiliza kwa makini, kukutana na hatimaye kutembea na Yesu.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakatekumeni kusikiliza kwa makini Mafundisho na ushuhuda juu ya Yesu wa Nazareti, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashahidi wake kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Yesu ndiye pekee anayeweza kuwapatia maana ya hija ya maisha yao hapa duniani.

Wanafunzi walipokutana na Yesu walitamani kubaki pamoja naye maisha yao yote, hii ina maanisha kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu ili kujenga na kuimarisha Jumuiya, kama njia ya kukutana na Mwenyezi Mungu anayemtafuta na kumwendea mwanadamu, ingawa mwanadamu daima anataka kumkwepa Mungu. Mwenyezi Mungu anapokutana na mwanadamu anapenda kujenga urafiki wa kudumu, ili mwanadamu aweze kuonja uwepo wake wa daima, kwa hakika Mungu ana kiu ya kukutana na Mwanadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika Wakatekumeni kufanya hija ya kutembea pamoja na Yesu kwani hiki ndicho kielelezo cha imani. Kuna wakati watasikia kuchoka au hata kupoteza dira na mwelekeo wa maisha, lakini kwa njia ya imani watambue kwamba, Yesu daima yuko pamoja nao na anawaalika kuingia katika Fumbo la Upendo wa Mungu, ili kuonja amani, utulivu na matumaini.

Baba Mtakatifu amewahakikishia Wakatekumeni msaada kutoka kwa Mama Kanisa katika hija ya maisha yao ya kiroho, huku wakitiwa shime kwa maombezi ya Bikira Maria. Kamwe wasipoteze ile sura ya Yesu aliyowaangali kwa mara ya kwanza na kuacha chapa ya kudumu katika maisha yao, kwa hakika Yesu ni mwaminifu katika ahadi zake, kamwe hawezi kuwadanganya!







All the contents on this site are copyrighted ©.