2013-11-24 08:03:17

Ushuhuda wa Wakatekumeni, jinsi walivyoguswa hata wakaamua kumfuasa Yesu katika hija ya maisha ya kiroho!


Katika Maadhimisho ya Kilele cha Mwaka wa Imani, Jumamosi jioni tarehe 23 Novemba 2013, Baba Mtakatifu Francisko amewapokea Wakatekumeni wanaojiandaa kupokea zawadi ya Imani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, kwenye Ibada ya Neno la Mungu iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amewapokea Wakatekumeni 500 kutoka katika nchi 47 waliokuwa wamesindikizwa na wazazi wao wa ubatizo pamoja na Makatekista wanaowandaa. Amewauliza maswali msingi na kile ambacho wanataka kutoka kwa Kanisa nao wakajibu kwamba, wanataka imani ili waweze kuwa na maisha ya uzima wa milele. Wakatekumeni ambao wameanza kutembea katika Mwanga wa Kristo mfufuka wametakiwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Neno la Mungu; kumtambua na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya maisha adili.

Haya ndiyo maisha ya Kanisa na kwamba, tangu sasa Kristo ndiye atakayekuwa kiongozi wa maisha yao. Baba Mtakatifu amewataka wazazi wa ubatizo na waamini katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba, wanawasaidia Wakatekumeni katika hija ya kumtafuta Kristo katika maisha yao.

Katika Ibada hii, wakatekumeni wametiwa ishara ya Msalaba kwenye njia za fahmu, ili Kristo awalinde kwa Ishara ya upendo wake mkuu, ili hatimaye, waweze kujifunza kumfahamu na kumfuasa. Ibada hii imekamilika kwa Wakatekumeni kuingia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro lililokuwa limefurika kwa umati mkubwa wa watu wakati huu Mama Kanisa anapohitimisha Mwaka wa Imani.

Wakatekumeni wameombewa ili waweze kupata msingi thabiti wa imani yao ndani ya Kanisa, wakionesha umoja na mshikamano; wakiendelea kuutafuta uso wa Yesu Kristo na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Waamini wawasaidie Wakatekumeni katika hija yao ya kiimani, daima wakiwa makini kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao wanapojiandaa kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu.

Kabla ya Ibada ya kupokelewa rasmi ndani ya Kanisa na Baba Mtakatifu, wakatekumeni walitoa ushuhuda jinsi walivyobahatika kupata cheche za imani ya Kikristo walipokuwa vyuoni, wakaguswa na Katekesi za kina zilizokuwa zinatolewa vyuoni humo; baadhi yao wamegundua furaha ya imani kutokana na matatizo na changamoto za kuondokewa na wazazi wao; upweke hasi uliopelekea jangwa la maisha ya kiroho; imani kwa Kristo kilikuwa ni kielelezo cha furaha na zawadi ya uhai waliyokirimiwa.

Mmong’onyoko wa maadili na tunu bora za maisha ya kiutu ni mambo yaliyochangia kwa baadhi yao kutafuta Mlango wa Imani, ili kuweza kukutana na Yesu Kristo, Mwalimu na Bwana wa maisha! Ni watu waliotamani kuonja fadhila ya imani, upendo na matumaini katika hija ya maisha yao! Baadhi ya vijana wanasema, waliguswa kwa namna ya pekee na ushuhuda maisha ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili hasa miongoni mwa vijana, wakapenda na kuamua kumfuasa Kristo!

Baadhi ya wakatekumeni wanasema, kwao imani ilikuwa ni kielelezo cha mwendelezo wa historia ya uwepo wa Mungu kati ya watu wake, wakataka kuonja mang’amuzi haya mapya! Kati ya wakatekumeni hawa, walionja Imani kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu, lakini matatizo na changamoto za maisha, zimewafanya wengi kumkimbilia Kristo.

Kwa upande wao, Makatekista wanasema, wameonja furaha ya imani kwa kuwasindikiza wakatekumeni katika majiundo ya maisha yao ya Kikristo, kiasi cha kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiroho na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa wanaishi Parokiani mwao!








All the contents on this site are copyrighted ©.