2013-11-23 14:07:04

Wahudumieni wagonjwa kikamilifu kwa kutambua na kuthamini utu, utambulisho na mahitaji yao msingi! Kamwe wasitengwe!


Wazee daima wamekuwa ni wadau wakuu katika maisha na utume wa Kanisa. Kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu, kuna haja kwa wakati huu, Kanisa kujitosa kimasomaso kuwasaidia wazee katika Jamii kwa kuibua mbinu mkakati makini, kwani wazee ni kielelezo cha hekima ya maisha, inayopaswa kurithishwa kwa wengine na kwamba, hawana budi kuhusishwa kikamilifu katika utume wa Kanisa. Maisha ya kila mtu yana thamani kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu, licha ya tabia za kibaguzi zinazoweza kuoneshwa na baadhi ya watu katika jamii.

Kutokana na maboresho ya huduma ya afya, watu wameendelea kuishi kwa muda mrefu zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa kwenye karne ya ishirini, hali ambayo inaambatana pia na shida pamoja na changamoto zake hasa magonjwa ya mishipa ya fahamu yanayowandama wazee kwa asilimia kubwa, kiasi hata cha kupoteza fahamu.

Magonjwa haya yanahitaji uwekezaji makini kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa hasa katika masuala ya tafiti, huduma na tiba muafaka kwa wagonjwa hao. Familia inabaki kuwa ni mahali pa faraja na ukarimu kwa wagonjwa.

Ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 23 Novemba 2013 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano wa XXVIII Kimataifa ulioandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, uliohitimishwa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, wagonjwa hawana budi kuhudumiwa kikamilifu, kwa kuheshimu na kuthamini utu, utambulisho na mahitaji yao msingi, bila kuwatenga wale wanaowahudumia, ndugu, jamaa na wafanyakazi katika sekta ya afya. Yote haya yanawezekana ikiwa kama kuna imani na hali ya kuheshimiana kati ya wadau mbali mbali. Kwa mwelekeo huu, huduma kwa wagonjwa inayotolewa kwa weledi mkubwa inagusa pia ubinadamu wao, vinginevyo, huduma kwa wagonjwa linakuwa ni jambo la mpito!

Baba Mtakatifu anawahimiza wafanyakazi katika sekta ya afya kuendeleza huduma makini kwa wagonjwa mintarafu mapokeo ya kitabibu, kwa kuboresha zaidi utu, uhuru na ukimya usiokuwa na maana ambao wakati mwingine unawaandama wale wanaofanya kazi ya huduma kwa wagonjwa. Baba Mtakatifu anawahimiza wafanyakazi hawa kuhakikisha kwamba, wanadumisha mwelekeo wa kidini na maisha ya kiroho kwa wagonjwa, hali inayobaki hata pale mgonjwa anapopoteza fahamu zake.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wahudumu katika sekta ya afya kuendeleza huduma ya maisha ya kiroho kwa wazee wagonjwa wanaokabiliwa na magonjwa ya mishipa ya fahamu, ili kuwasaidia kuendeleza uhusiano na majadiliano na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kuwatakia kheri na baraka wazee waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia. Wafanyakazi katika sekta ya afya watambue pia kwamba, ni sehemu ya wadau wa Uinjilishaji kwa njia ya sakramenti ya Ubatizo waliyoipokea. Kila siku ya maisha yao, wanapaswa kuwa ni mashahidi wa Kristo katika sehemu mbali mbali za maisha ya mwanadamu na kwa njia hii, watu wanaweza kumfahamu na kumpenda Kristo na Injili yake hasa miongoni mwa vijana. Baba Mtakatifu amewaweka wajumbe hao chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria msaada wa wagonjwa.







All the contents on this site are copyrighted ©.