2013-11-23 11:38:17

Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya kukutana mwakani kuzungumzia masuala ya tabianchi!


Mratibu wa Kamati ya Mazingira ya Viongozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) - (CAHOSCC) - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amependekeza kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa nchi za AU na Umoja wa Ulaya (EU) kujadili na kufikia msimamo wa pamoja kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Nchi za Ufaransa na Uingereza zimekubali kwa furaha pendekezo hilo na zimeahidi kuwa zitaanza kulifanyia kazi pendekezo hilo miongoni mwa nchi wanachama wa EU wakati Rais Kikwete atashughulika kuwaratibu viongozi wenzake wa AU kuhusu mkutano huo unaopendekezwa kufanyika mwakani.

Rais Kikwete alitoa pendekezo hilo Alhamisi, Novemba 21, 2013, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Mheshimiwa Fabius na Waziri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi za Uingereza, Mheshimiwa Ed Davey. Rais Kikwete alikutana na mawaziri hao mjini Warsaw, Poland ambako wote watatu walikuwa wanahudhuria Mkutano wa Mabadiliko ya Taiba Nchi duniani – COP19/CMP9- uliomalizika jana kama mawaziri na maofisa waandamizi wa nchi mbalimbali wanaoendelea na majadiliano ya kutafuta mwafaka katika masuala mbalimbali yanayohusu jambo hilo hadi Jumapili, Novemba 24, 2013.

Katika mikutano tofauti, mawaziri hao walikubaliana na pendekezo la Rais Kikwete kuwa ni muhimu kwa nchi wanachama wa AU na EU kufanya mkutano wao ili kuandaa msimamo wao kwa ajili ya Mkutano wa COP20/CMP10 uliopangwa kufanyika Paris, Ufaransa. Inatarajiwa kuwa itakuwa kwenye mkutano wa Paris ambako nchi mbali mbali duniani zitatia saini mkataba wa kisheria wa kusimamia mabadiliko ya tabia nchi duniani. Hivyo, mkutano ambao amependekeza Rais Kikwete utalenga kuziwezesha nchi za Afrika na EU kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu baadhi ya masuala muhimu yanayohusiana na suala zima la mabadiliko ya tabia nchi.

“Sisi ndani ya AU tunaona kuwa tuko karibu zaidi na misimamo ya EU kuhusu mambo mengi yanayohusiana na suala zima muhimu la mabadiliko ya taiba nchi,” Rais Kikwete alimwambia Waziri Fabius katika mkutano wao uliofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Warsaw ambako ndiko mkutano huo ulikokuwa unafanyika. Waziri Fabius alifuatana na mawaziri wenzake wawili wa Ufaransa - Waziri wa Mazingira na Waziri wa Misaada ya Kimataifa ya Maendeleo.

Katika mkutano wake na Waziri Davey, kwenye Hoteli ya Bristol, Rais Kikwete alisema: “Nimekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa. Nimependekeza mkutano wa pamoja na viongozi wa AU na EU ili tupate nafasi ya kujadili na kufikia makubaliano katika maeneo mbali mbali ya suala zima la mabadiliko ya tabia nchi. Mkutano huu utatuwezesha kujua wapi tunakubaliana, wapi tuna tofauti na zipunguzwe namna gani. Nataka kutoa pendekezo hilo kwako wewe Mheshimiwa Waziri.”

Mheshimiwa Davey ambaye anaajitambulisha kama mwanamazingira wa maisha alionekana kufurahishwa na pendekezo hilo la Rais Kikwete na akasema: “Umekamilisha siku yako vizuri sana. Naunga mkono pendekezo hilo moja kwa moja.”

Teteeni nchi badala ya kuiponda kwenye mablogu, Rais Kikwete awaambia Watanzania waishio nje
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema wajibu mkuu wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni kuisemea vizuri, kuihangaikia na kuitetea nchi badala ya kushinda kwenye mablogu wakiiponda, kuibeza na kulalamika. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kuishi kwa Watanzania nje ya nchi kutaonekana jambo la maana zaidi ikiwa watatumia rasilimali na fursa wanazozipata ugenini kusaidia kubadilisha hali na maisha ya ndugu zao waliobakia Tanzania.

Rais Kikwete pia amewaonya Watanzania hao wasije kuchanganyikiwa na kujichanganya wenyewe kwa kuiga tamaduni za kigeni kupita kiasi. Rais Kikwete alikuwa anazungumza na Watanzania waishio nchini Poland, Alhamisi, Novemba 21, 2013, kwenye Hoteli ya Bristol mjini Warsaw ambako alifikia wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku nne katika Poland.

Aliwaambia Watanzania hao na familia zao: “Matumaini na matarajio yetu sisi tuliobakia nyumbani ni kwamba mtaisemea vizuri nchi yetu, mtaitetea nchi yenu, mtaihangaikia nchi na kuleta faida nyumbani. Ni jambo haliingii akilini kuwa baadhi yenu mnaweza kuishi hapa na kazi yenu ikawa ni kushinda kwenye mablogu mkilaumu nchi yenu wenyewe. Nchi mbaya, viongozi hawafai..mnapata faida gani. Mnazo nchi ngapi?”

Aliongeza Rais Kikwete: “Kuhangaikia nchi yetu ni wajibu wenu ambao hamwezi kuukwepa. Matumaini yetu ni kwamba mtasukuma mbele maslahi ya nchi yenu, mtatetea ustawi wa nchi yenu na ndugu zenu. Fursa zilizoko hapa mnazijua wenyewe, sisi hatuzijui. Nyie ndio mnaishi hapa, sisi tuko mbali na hatuwezi sisi kutegemewa na kutarajiwa tufanye mambo ya hapa ambayo hatuyajui.”

Alisisitiza Rais Kikwete: “Mbona kazi za ma-Ngo’s mnazifanya vizuri bila kusukumwa ama kushawishiwa lakini kazi za kusaidia ndugu zenu hamfanyi? Kama hata hamwezi kusaidia ndugu zenu mnachangia nini nchi yenu?” Rais amesema kuwa kwa Watanzania waishio nje kuonekana wanajali na kutetea nchi yao kutasaidia kujenga hoja ya msingi kuhusu umuhimu wa kuanzishwa kwa uraia pacha (dual citizenship) ambao Watanzania waishio nje wanaulilia. “Mnaweza kuhalalisha hoja ya uraia pacha kwa kuwa watu wenye faida kwa nchi.”

Kuhusu ombi lao la uraia pacha, Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa Watanzania waishio nje kuongeza kasi ya kuchangia mjadala kuhusu suala hilo ili likubaliwe kuingizwa kwenye Katiba Mpya. “Rasimu ya kwanza ya Katiba ililikataa jambo hilo kwa sababu hili ni jambo lisilokuwa na ushabiki na upenzi mwingi nyumbani. Ujumbe wangu kwenu ni jipangeni vizuri kutetea hoja yenu hii. Saidieni mjadala wa jambo hilo badala ya kushinda kwenye mablogu mkijadili siasa na hivyo kusahau yenye maslahi kwenu.”

Kuhusu kuiga tamaduni za nchi nyingine na kusahau za nyumbani, Rais Kikwete aliwaambia kuwa inaelekea kuwa baadhi wachache wanaoishi nje ya nchi, wamejichanganya na kuchanganyikiwa kiasi cha kusahau mambo ya kwao. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya mmoja wa Watanzania kudai kuwa suala zima la mahari limepitwa na wakati na kuwa kutoa mahari ni sawa ni kuwauza watoto wa kike. Rais ambaye alionyesha kushangazwa na kauli hiyo, alijibu: “Msiige mambo ya kigeni kiasi cha kuanza kuchanganyikiwa.”








All the contents on this site are copyrighted ©.