2013-11-23 09:19:28

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaendelea kuyachangamotisha Makanisa ya Mashariki kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, Umoja na Ushuhuda wa imani katika matendo!


Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki hapo tarehe 22 Novemba 2013 limehitimisha mkutano wake wa Mwaka uliofunguliwa tarehe 19 Novemba 2013 kwa kuwashirikisha wakuu wa Makanisa kutoka Mashariki pamoja na viongozi waandamizi kutoka Vatican.

Wajumbe wa mkutano huu wamepata fursa ya kupembua mawazo makuu yaliyojitokeza tangu Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusiana na Makanisa ya Mashariki hadi nyakati hizi. Mkutano umeendeshwa katika hali ya utulivu na amani na hivyo kutoa fursa kwa wajumbe kushirikishana mang'amuzi ya maisha na utume wa Makanisa ya Mashariki; kusikiliza kwa makini na kuchangia kwa umakini mkubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Makanisa ya Mashariki.

Waamini kutoka katika Makanisa haya wameathirika kwa namna ya pekee na vita; ukosefu wa uhuru wa kuabudu, madhulumu na nyanyaso za kidini zilizopelekea makundi makubwa ya waamini kuzikimbia nchi zao ili kusalimisha maisha yao. Waamini hawa wakaonja upendo na huruma kutoka kwa waamini wa Makanisa yenye madhehebu ya Kilatini; wakapewa nyumba za Ibada na kutambuliwa uwepo wao!

Licha ya tofauti ya Kanuni na Sheria za Kanisa, wajumbe kwa pamoja wamepongeza utekelezaji wa maamuzi makuu yanayofanywa kwa njia ya Sinodi za Mapatriaki, sanjari na mwendelezo wa majadiliano ya kina na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama alivyofanya tarehe 21 Novemba 2013 kwa kuzungumza na Mapatriaki, Maaskofu wakuu pamoja na wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki.

Wajumbe wa mkutano huu wameguswa kwa namna ya pekee na Mafundisho juu ya Kanisa kama yalivyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa kukazia majadiliano ya kidini na kiekumene ili kukuza na kudumisha umoja katika tofauti; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati; daima Makanisa ya Mashariki yakijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Wajumbe wamegusia pamoja na mambo mengine kuhusu halisi ya kitume, tatizo na changamoto ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum; uwepo wa Wakristo Mashariki ya Kati na changamoto zake pamoja na kuangalia umuhimu wa kuwa na vongozi wa Kanisa mahali ambapo kuna makundi haya ili yaweze kupata huduma za maisha ya kiroho hata pale wanapokuwa ugenini kwa kuzingatia kanuni, sheria na Mapokeo ya mahali wanapotoka.

Wajumbe wameonesha umuhimu wa kujenga miundo mbinu kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa waamini wa Makanisa ya Mashariki mintarafu changamoto za Uinjilishaji Mpya, kwa kuzingatia pia Mapokeo ya maisha ya kiroho na Liturujia ya waamini kutoka katika Makanisa yao. Kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo kadiri ya utashi wa Kristo, ili wote wawe wamoja chini ya Kristo Mchungaji mkuu, kwa kuendeleza ushuhuda na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Wajumbe wanasema, viongozi wa Makanisa ya Mashariki waendelee kuongoza, kuadhimisha Liturujia na ufahamu wa Fumbo la Kristo, mintarafu taalimungu na Kanuni ya Imani ya Costantinopoli. Makanisa ya Mashariki na Magharibi kwa pamoja yanaendelea kuchangamotishwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kidini katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Wawe ni mashahidi wa upendo wa Kristo katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu na kwamba, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.