2013-11-23 12:27:24

Marufuku kujisajili kwenye Ufalme wa Shetani!


Wapendwa wanafamilia ya Mungu, karibuni kwa tafakari ya Neno la Mungu, inayotujia tunapoadhimisha leo Sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme. Mama Kanisa anatualika tumtafakari Kristo ambaye ni Mfalme wa Ulimwengu na pia kielelezo halisi cha Mfalme wa kweli ambaye ni tofauti na wafalme wa dunia hii. RealAudioMP3


Tofauti na miaka mingine, kwa mwaka huu adhimisho hili la Sherehe ya Kristo Mfalme linaambatana na hitimisho rasmi la Mwaka wa Imani. Hivyo ni nafasi nzuri kwetu kujikumbusha kuwa Imani ya kweli ni ile ambayo inajengeka katika Kristo Mwenyewe ambaye atatupa tuzo la kushiriki maisha katika ufalme wake wa mbinguni kadiri ile ambavyo tumejibidisha kuiishi imani yetu na kwa jinsi tulivyomruhusu awe Bwana na Mtawala wa maisha yetu.


Kihistoria, sherehe hii ilianzishwa na Papa Pius XI mwaka 1925 akitaka kumtambulisha Kristo kuwa ndiye mfalme wa kweli tofauti na wafalme dhalimu wa nyakati hizo, na kuwakumbusha wanadamu kuwa amani, furaha, na upendo wa kweli kwa mwanadamu vinapatikana kwa kumruhusu Kristo atawale maisha yetu. Mtawala yeyote wa dunia hii, pamoja na heshima halali anazostahili kupewa, kamwe asitazamwe kuwa ndio ukomo wetu, bali mwanzo na ukomo wetu ni Kristo Mwenyewe ambaye ni Bwana na Mfalme.


Tangu mwaka 1925 Sherehe hii iliadhimishwa Jumapili ya Mwisho ya Mwezi Oktoba iliyotangulia Sherehe ya Watakatifu wote hadi mwaka 1969 ambapo Papa Paul VI aliipa tarehe mpya na kuanza kuadhimishwa katika Jumapili ya Mwisho wa Mwaka wa Kanisa hadi leo hii. Tunaiadhimisha Sherehe hii Jumapili ya Mwisho wa Mwaka wa Kanisa kuashiria kuwa Kristo ni Mfalme wa Nyakati zote atakayekuja mara ya pili kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu; huku tukitazamia kuanza kipindi cha Majilio - ambapo tunatazamia ujio wa kwanza wa Kristo kama Masiha.


Maandiko Matakatifu kutoka katika masomo ya Jumapili hii, yanatuongoza na kutusaidia kutafakari kwa undani zaidi juu ya fundisho hili juu ya Ufalme wa Kristo na namna ambavyo Kristo anavyojidhihirisha kuwa Mfalme wa pekee sana, tofauti na wafalme wa dunia hii, na kutoa changamoto kwetu jinsi ya kushiriki maisha katika ufalme huo kwa kumruhusu Krito atawale maisha yetu.


Injili ya leo inatupeleka mpaka Kalvari ambapo tunamwona Kristo akiwa ameangikwa Msalabani, anathibitisha kuwa Yeye ni Mfalme na Bwana wa Uzima hasa kwa kumwahidia Uzima wa Milele yule “mwizi aliyetubu” – ambaye ni yeye pekee kati ya wale wote waliomzunguka pale Msalabani aliyeweza kukiri na kumshuhudia kuwa hakika Kristo ni Mfalme.

Kristo anajitambulisha kuwa yeye ni Mfalme Mnyenyekevu na asiyependa sifa wala makuu; kwa kutokuwa tayari kukidhi kiu ya wale waliomkejeli na kumkashifu pale Msalabani kwa kumtaka jinsi ile ile alivyowaokoa wengine vivyo hivyo ajiokoe mwenyewe. Aidha, anajidhihirisha kwetu kuwa ni Mfalme mwenye kusamehe: akiwasamehe kuanzia wale waliokuwa wanamkashifu pale Msalabani, na zaidi sana yule mwizi ambaye kwa hakika alipata wokovu hatua za mwishomwisho. Kristo anasamehe pasipo kujali uzito wa dhambi bali anatazama uthabiti wa toba ya mtu.


Somo la kwanza, linaeleza juu ya kutawadhwa kwa Mfalme Daudi ambako kunaambatana na tendo la kupakwa mafuta. Ni kutoka katika Ukoo huu wa Kifalme ndipo anazaliwa Kristo Masiha na ambaye ni Mfalme: tena Mfalme wa Mbingu na Dunia na wa Milele tofauti na alivyokuwa Daudi na wafalme wengine wa dunia hii.


Katika Somo la Pili, Mtume Paulo anamtambulisha kwetu Yesu Kristo Mfalme wa Milele, aliye asili ya vitu vyote, anayetukomboa kutoka katika giza na kutuingiza katika nuru, kwake tunapata msamaha wa dhambi zetu, tunapata amani kutokana na kifo chake Msalabani na kufunguliwa mlango wa mbingu kwa ufufuko wake. Kristo ni mtangulizi wetu katika yote, na hivi tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu!


Kutokana na utajiri huo tunaoupata kutoka katika masomo ya leo, tunaona dhahiri kuwa Bwana wetu Yesu Kristo ni Mfalme wa pekee kwani: ni Mfalme wa amani, wa haki, mwenye upendo kwa wote, mtumishi na sio mtumikiwa, mnyenyekevu na si mpenda makuu, mwamuzi mvumilivu na mwenye huruma wala asiye mwepesi wa hasira; kiongozi na si mwenye kuamuru tu, mwenye kusamehe na sio kulipiza kisasi; Mchungaji na sio mpenda madaraka, anayehangaikia uzima na ustawi wa watu wote pasipo kuendekeza ubinafsi, na ambaye ufalme wake ni wa nyakati zote.


Hivyo katika Jumapili hii, tunapewa changamoto ya kufanya uchaguzi huru wa ama kumfuata Kristo Mfalme au kinyume chake, yaani, kufuata ufalme wa mwovu shetani. Tutadhihirisha tu kuwa tunamfuata Kristo Mfalme kwa maisha yetu, jinsi ambavyo tunaziishi hizo tunu njema zinazoutambulisha ufalme wake.


Vinginevyo tutakuwa tumejisajili katika ufalme wa shetani kama tutaruhusu maisha yetu yatawaliwe na matendo maovu kama vile: ubinafsi, chuki, vita, kutothamini uhai, kupoteza ladha ya masuala yanayomuhusu Mungu, kutekwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kumsahau Mungu; utoaji mimba, ndoa za jinsia moja, uvunjifu wa ndoa, ukosefu wa malezi bora katika familia, kuhalalisha dhambi na kutoona thamani ya toba, unyanyasaji, uchu wa mali na madaraka, na mengine kama hayo tunayoyashuhudia katika ulimwengu wetu wa leo.


Wapendwa wanafamilia ya Mungu, ninapenda kuhitimisha tafakari hii kwa kumwalika kila mmoja wetu amshukuru Mungu kwa zawadi ya mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo – ambaye amemtuma ili atawale na kuongoza maisha yetu, tunaposafiri kuelekea mbinguni. Aidha, tunapohitimisha leo adhimisho la Mwaka wa Imani, tuendelee kujiombea sisi wenyewe, kwanza: msamaha kwa jinsi ambavyo mara nyingi tumeisaliti imani yetu kwa kuishi kinyume na matakwa ya ufalme wa Kristo.

Pili, tumwombe Mungu ili tudumu siku zote katika imani kwake. Tuwaombee wale wengine ambao hawajapata bado kuisikia sauti ya Kristo na zaidi sana wale ambao wamejitenga na ufalme wa Kristo ili wapate kurudi, na hatimaye, sote tuweze tena kuwa kundi moja chini ya Mchungaji na Mfalme mmoja, Bwana wetu Yesu Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na: Pd. Kwene Alfred,
Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.