Yesu Kristo ni Mfalme wa ukweli na uzima; utakatifu na neema; haki, mapendo na amani!
Askofu mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano na Radio
Vatican wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kufunga Mwaka wa Imani sanjari na Siku
kuu ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu
sifa na ukuu unaosimuliwa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Kristo
Mfalme, hili ujumbe huu uweze kuwa kweli ni dira na mwongozo katika mchakato wa kuyatakatifuza
malimwengu.
Yesu Kristo ni Mfalme wa ukweli, waamini wanachangamotishwa na
Mama Kanisa kuwa kweli ni wajumbe wa ukweli. Yesu ni Mfalme wa uzima anayewakirimia
waja wake maisha tele! Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kukumbatia
na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji
mimba, nyanyaso, madhulumu pamoja na kutothamini utu na heshima ya binadamu.
Yesu
Kristo ni Mfalme wa Neema na kwamba, yuko tayari kuwakirimia waja wake neema na baraka
wanazohitaji katika hija ya maisha yao hapa dunia, ikiwa kama watakuwa na moyo radhi,
tayari kumsikiliza kutoka katika undani wa maisha yao. Kwa sifa hizi, Askofu mkuu
Lebulu anawataka waamini wakati huu Mama Kanisa anapoufunga Mwaka wa Imani, kuzipatia
sifa hizi umuhimu wa pekee katika vipaumbele vya maisha yao kama sehemu ya mchakato
wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha matakatifu na adili.