2013-11-22 15:31:47

Ugeni mzito kutoka China unatembelea Tanzania


Katika juhudi zinazoendelea za kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Serikali za Mitaa za Tanzania na China. Jumla ya wageni wapatao 70 kutoka Serikali za Mitaa za China, wakiwemo Magavana, Mameya na Wafanyabiashara wanatarajiwa kuzuru Tanzania kuanzia tarehe 23 Novemba hadi tarehe 26 Novemba mwaka 2013.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) alisema ujumbe huo utakuwepo nchini ikiwa ni ziara maalum iliyoandaliwa na Ofisi Waziri MKuu-TAMISEMI kwa lengo la kudumisha ushirikiano katika masuala ya Serikali za Mitaa. Wageni hao watakutana na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda, baadhi ya Mawaziri wa Sekta mbalimbali, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa.

Wengine watakaokutana nao ni baadhi ya Mameya/Wenyeviti wa Halmashauri za Jiji, Manispaa, Miji na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri,Taasisi za Serikali na Binafsi pamoja na Wafanyabiashara. Lengo la ujio huo ni kuanzisha rasmi ushirikiano kati ya Serikali za Mitaa za Tanzania na China kupitia Shirikisho la Ushirikiano wa Serikali za Mitaa za Afrika na China. Kupitia Umoja huo ushirikiano kati ya Serikali za Mitaa za Tanzania na China utakuwa wa Kimkakati zaidi.

Ziara hii itafungua ukurasa mpya wa urafiki na kusaidia kuleta maendeleo na huduma nzuri za kijamii. Aidha, utaendeleza urafiki wa Tanzania na China pamoja na kudumisha utamaduni wa kubadilishana uzoefu wa kuwahudumia wananchi kupitia Serikali za Mitaa.

Maeneo ambayo China na Tanzania wamekwishakubaliana katika mahusiano yao ni pamoja na Ujenzi au Ukarabati wa Miundombinu, Ujenzi na Uendelezaji wa maeneo ya biashara, Ujenzi na uendelezaji wa Standi kubwa za kisasa za mabasi, uendelezaji wa maeneo makubwa ya wazi, upangaji Miji, Mafunzo maalum ya utunzaji wa mazingira na kutoa misaada ya kifedha kwa njia mbalimbali katika maeneo mbalimbali.

Ili kufanikisha ziara hii, Serikali Kuu imewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi zilizoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI kubaini fursa za uwekezaji na kuandaa Mipango yao ya kuanzisha miradi ya kimaendeleo katika maeneo husika ya makubaliano na China ili makubaliano hayo yaanze kutekelezeka.

Matokeo ya ziara hii ni Tanzania kupata fursa ya kunufaika katika maeneo ya Uchumi, Biashara Elimu ya Jamii, Sayansi, Tekinolojia, Utamaduni na maeneo mengine mbalimbali ambayo yatarahisisha zaidi kufanikisha na kudumisha urafiki kati ya Tanzania na China. Maeneo meingine yatakayotembelewa na ujumbe huo ni pamoja Makumbusho ya Taifa, Reli ya TAZARA, eneo la Uwekezaji la EPZ, Wizara ya Ujenzi, Wakala wa Ujenzi (TANROADS), Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Uchukuzi.

Aidha, katika kuimarisha ushirikiano huu, Serikali ya China itawazadia tuzo wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao wapatao 200 kati yao wanafunzi 100 ni kutoka Shule za Sekondari na wengine 100 kutoka shule za Msingi ambapo wanafunzi kutoka Sekondari watazawadiwa kiasi cha Tsh. 250,000/= na kutoka shule za msingi watazawadiwa Tsh.125,000/=.

Chimbuko la Mahusiano hayo lilitokana na mkutano wa uzinduzi wa Shirikisho la ushirikiano kati ya Serikali za Mitaa za China na Afrika uliofanyika tarehe 28/08/2012 wakati wa Mkutano wa kwanza wa Shirikisho hilo uliofanyika Beijing China.








All the contents on this site are copyrighted ©.