Tunu msingi za mchezo wa rugby ziwawezeshe wanamichezo kufikia lengo kuu la maisha!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013 amekutana na kuzungumza na
wachezaji wa timu za rugby kutoka Italia na Argentina. Amewashukuru na kuwapongeza
kwa moyo wa urafiki unaojionesha baina ya mataifa haya mawili katika michezo ambayo
wakati mwingine inalenga kusaidia kugharimia matendo ya huruma.
Baba Mtakatifu
anasema rugby ni mchezo wa kupimana nguvu, unaohitaji kuheshimiana sanjari na kudhibiti
tabia ya mtu binafsi na utashi kwani hapa "si maji kwa glasi kani yataka moyo kweli
kweli" Ni mchezo unaopania kufikia lengo, kwani hata maisha ni mapambano yenye malengo,
yanayohitaji moyo wa ushirikiano na mshikamano, kwa kusaidiana, ili kwa pamoja wote
waweze kusherehekea ushindi.
Baba Mtakatifu anasema, si mtaalam sana wa mchezo
wa rugby, lakini kama Askofu anauangalia mchezo huu kwa jicho la Kiinjili na kuwataka
kuhakikisha kwamba, tunu msingi wanazozitumia katika mchezo wa rugby wanazitumia pia
katika hija ya maisha yao nje ya uwanja wa rugby.