Mshikamano wa upendo na wananchi walioathirika kwa majanga asilia wakati wa kufunga
Mwaka wa Imani mjini Vatican
Katika Maadhimisho ya Kilele cha Kufunga Mwaka wa Imani, Jumapili ijayo kwenye Kanisa
kuu la Mtakatifu Petro, waamini na watu wenye mapenzi mema watachangia sadaka itakayopelekwa
nchini Ufilippini ili kusaidia watu waliokumbwa na majanga nchini humo, kama kielelezo
makini cha mshikamano na watu wenye shida mbali mbali Mama Kanisa anapofunga rasmi
Mwaka wa Imani.
Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na
watu wasiokuwa na makazi maalum linasema kwamba, kunako Mwaka 2004 na Mwaka 2011 mchango
kama huu ulikusanywa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Asia Kusini waliokumbwa na
Tsunami na baadaye wananchi wa Japan walipokumbwa na mafuriko yaliyosababisha maafa
makubwa.
Msaada huu unasimamiwa na kuratibiwa na Utume wa Bahari kwa ajili
ya nchi zilizoathirika kwa majanga asilia. Kanisa Katoliki kwa njia ya mashirika yake
ya misaada linaendelea kuwafariji waathirika kwa hali na mali. Msaada huo pamoja na
mambo mengine, utakuwa ni kielelezo halisi cha mshikamano wa dhati katika ujenzi wa
makazi, ununuzi wa vifaa vya uvuvi na huduma ya elimu kwa watoto yatima na wale wanaoishi
katika mazingira hatarishi.