2013-11-22 09:31:46

Je, ni kwa nini yote haya yatokee nchini Ufilippini! Hii ndiyo Sala ya Kwanini!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 21 Novemba 2013 alikutana na kuzungumza na Waamini kutoka Ufilippini wanaoishi mjini Roma waliokuwa wameandamana na Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, kwa ajili ya kubariki Picha ya Mtakatifu Pedro Calungsod aliyeishi kati ya Mwaka 1654 hadi mwaka 1672.

Alikuwa ni Katekista mahiri kutoka Ufilippini, aliyeungama imani yake kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya kifodini. Akatangazwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kuwa Mtakatifu hapo tarehe 21 Oktoba 2012. Waamini kutoka Ufilippini baada ya Baba Mtakatifu Francisko kubariki picha hii, waliendelea na Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amemshukuru Kardinali Tagle kwa moyo mkuu na wenye uvumilivu hasa wakati huu Ufilippini inapoendelea kukabiliana na athari za majanga yaliyojitokeza hivi karibuni nchini humo na kusababisha maafa makubwa kwa maisha na miundo mbinu. Wananchi wengi wameweza kukabiliana na hali hii kwa imani na matumaini na kwamba, kwa sasa wanahitaji kuonjeshwa moyo wa mshikamano na upendo. Kuna mambo mengi ambayo yanaendelea kubaki kuwa ni fumbo kwa maisha ya mwanadamu hapa duniani.

Katika majonzi na simanzi zote hizi, wananchi wa Ufilippini waendelee kusali na kumuuliza Mwenyezi Mungu, Je, maana yake nini mambo haya yote? Baba Mtakatifu amehitimisha maneno ya faraja kwa waamini kutoka Ufilippini kwa kuwahakikishia kwamba, yuko pamoja nao katika shida na mahangaiko yao. Baadaye, akabariki Picha ya Mtakatifu Pedro Calungsod, Katekista shupavu na Shahidi mwaminifu kwa Injili ya Kristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.