2013-11-22 09:08:27

Bikira Maria ni Mama wa Matumaini! Je, bado taa ya matumaini inaendelea kuwaka katika Monasteri?


Shamrashamra za kufunga Mwaka wa Imani sanjari na Sherehe za Kristo Mfalme zimeanza kutimua vumbi mjini Vatican baada ya Baba Mtakatifu Francisko. Alhamisi tarehe 21 Novemba 2013 kuwatembelea na kusali pamoja na Wamonaki wa Shirika la Wakamadoli mjini Roma.

Baba Mtakatifu aliongoza Ibada ya Masifu ya Jioni na baadaye Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya aliongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kama changamoto kwa waamini kumkaribisha Kristo katika hija ya maisha yao ya ndani.

Katika tafakari yake, Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria alionesha upendo mkuu kwa Yesu na akajitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika hija ya maisha yake hapa duniani, kiasi kwamba, akawa ni Mama wa Mkombozi na Mwanafunzi amini wa Kristo, aliyejiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kielelezo cha mtu mwenye matumaini thabiti.

Bikira Maria alikubali mpango wa Mungu katika maisha yake tangu siku ile alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Hakufahamu undani wa Fumbo la Umwilisho, lakini akalisubiri kwa moyo wa matumaini, hata siku ile Masiha alipozaliwa katika hali ya umaskni, lakini hata katika mazingira kama haya, hakukata tamaa, ingawa siku ile Yesu alipokuwa anatolewa Hekaluni, Wazee Simeoni na Anna walimwambia kwamba, upanga utaingia moyoni mwake, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Utume wa Bikira Maria katika historia ya ukombozi kwa kiasi fulani unafanana na utume wa Yesu katika Fumbo la Ukombozi.

Baba Mtakatifu anasema, licha ya magumu na changamoto zote hizi, bado Bikira Maria aliendelea kuwa ni mwanamke wa matumaini aliyeyarutubisha kwa njia ya kusikiliza kwa makini Neno la Mungu; akalitafakari kwa unyenyekevu na kulimwilisha kwa njia ya matendo ya huruma, pale mjini Kana, wanaharusi walipotindikiwa na divai. Hapa akamtambulisha Yesu kuwa ni Mwalimu na Masiha. Bikira Maria akayahifadhi matukio yote haya katika sakafu ya moyo wake mtakatifu. Mwanaye mpendwa Yesu akaonekana kuwa kweli alama ya kusimama na kuanguka kwa wengi, kama ilivyokuwa imetabiriwa.

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria chini ya Msalaba akalitafakari Fumbo la Pasaka kwa uchungu na kwa wale waliokata tamaa wangeweza kusema, hapa matumaini ya Bikira Maria yalizimika kama kibatari! Lakini, Bikira Maria ni Mama wa Imani thabiti, akaendelea kusadiki katika mpango wa Mungu bila kuyumba wala kuteteleka! Bahati mbaya, binadamu wa leo anataka muujiza mara moja, hana tena subira ya kusubiri ile Alfajiri, Siku ya kwanza ya Juma! Pale kaburini, taa iliyokuwa inawaka ilikuwa ni ya Mama Bikira Maria, tumaini kwa familia yote ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anauliza, Je, hata leo hii taa ya matumaini bado inawaka kwenye Monasteri?, Je, wanaendelea kusubiri Mpango wa Mungu katika maisha yao? Bikira Maria aliyejipambanua katika historia ya wokovu ni shahidi makini wa tumaini, anayewaenzi watoto wake wakati wa shida na magumu; anawafariji pale wanapoonekana kana kwamba, yote yamekwisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.