2013-11-21 11:33:34

Watu wanataka kuona ukweli na uwazi katika usimamizi wa mali ya Kanisa na matumizi yake kwa maskini!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 21 Novemba 2013 amekutana na kuzungumza na Mapatriaki pamoja na Maaskofu wakuu kutoka Makanisa ya Mashariki wanaohudhuria mkutano ulioandaliwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema kama viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa waaminifu kwa Kristo, Kanisa na Watu wote.

Watambue kwamba, wao ni walinzi na wahudumu wa umoja wa Kanisa unaojionesha kwenye Makanisa mahalia, zawadi ya Roho Mtakatifu kwa kuungana pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama kielelezo makini cha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Umoja huu unapaswa kuimarishwa kwa njia ya Sinodi za Mapatriaki.

Baba Mtakatifu anasema, ili ushuhuda wao kama viongozi uweze kuaminika wanapaswa daima kutafuta: haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole, kwani wamejua neema ya Yesu jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yao, ingawa alikuwa tajiri ili wao waweze kuwa matajiri kwa umaskini wake. Ni viongozi wanaopaswa kutekeleza wajibu wao kwa ari na moyo mkuu kwa kuonesha upendo, udugu na ubaba kati ya Familia ya Mungu wanayoiongoza, lakini zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee Makleri wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha, kwani hawa wana haki ya kuonjeswa mfano mzuri kuhusiana na mambo ya kimungu na maisha ya Kanisa. Wanahitaji kuona ukweli na uwazi katika usimamizi wa mali ya Kanisa na matumizi yake kwa maskini sanjari na utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Sinodi ya Mapatriaki







All the contents on this site are copyrighted ©.