Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi leo amewaongoza mamia ya wanajumuiya wa
chuo kikuu cha Mt. Yohana Tanzania chenye makao yake makuu mjini Dodoma kushiriki
ibada takatifu ya kuomboleza kifo cha makamu mkuu wa chuo hiko marehemu Prof. Gabriel
Mwaluko.
Ibada hiyo takatifu ya maombolezo ilifanyika kwenye ukumbi wa chuo
hiko mjini Dodoma ambapo ilihudhuriwa na uongozi na wanajumuiya wa chuo iko, ibada
hiyo pia ilitumika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa utumishi aliompa marehemu Prof. Mwaluko
chuoni hapo, kwenye taasisi mbalimbali na kuitumikia jamii kwa ujumla enzi za uhai
wake.
Akitoa taarifa kwenye ibada hiyo Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Mt. Yohana
Dr. Asad Kipanga alisema takribani miezi miwili marehemu Prof. Mwaluko alikuwa nchini
India kwa matibabu na kwa kipindi chote hiko chuo kimekuwa na mawasiliano ya karibu
na familia ya Prof. Mwaluko na walitarajia Prof. angerejea salama nchini siku za hivi
karibuni lakini hali haikuwa hivyo.
Kwa upande wake mlezi wa kiroho chuoni
hapo, Askofu Francis Ntiruka akiongoza ibada hiyo amebainisha kua chuo na jumuiya
yake nzima imepata pigo kubwa na ameeleza watamkumbuka marehemu Prof. Mwaluko kama
mtu wa imani kupitia maisha na matendo yake, pia atakumbukwa kujitolea kwake katika
kazi na hamasa yake. Askofu Ntiruka ametoa rai kwa viongozi wa mataifa ya leo kuwa
endapo watatumika kwa kujitoa uongozi wao utadumu, utaheshimika na kukumbukwa daima
ambapo alimtolea mfano baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi aliyewaongoza wanajumuiya wa chuo kikuu
cha Mt. Yohana katika ibada hiyo amesema serikali imepokea msiba chuo wa prof. Mwaluko
kwa majonzi na masikitiko kwa kutambua umuhimu aliokuanao Prof. Mwaluko kwenye hatua
ya maendeleo iliyokuwa ikipitiwa na chuo hiko kwa sasa na kuongeza kuwa serikali inakitazama
chuo hiko kwa upekee kwa mchango wake wa kuandaa wataalamu waliojifunza kuihudumia
jamii kwa uadilifu.