2013-11-21 09:00:32

Ndugu zake Kristo ni wale wanaotekeleza mapenzi ya Mungu na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha!


Waamini wanaalikwa kujenga na kuimarisha Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, kwa kuungama imani kwa Mungu mmoja, Mtakatifu, mwenye nguvu na mweza wa yote, kwani hii ndiyo imani inayofumbatwa na Kanisa katika Fumbo la Utakatifu Mtakatifu.

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 21 Novemba, Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, sanjari na Siku maalum kwa ajili ya kuwaombea Wamonaki wanaojitoa kwa sala na tafakari kwa Mungu na ustawi wa Kanisa.

Kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria, waamini wanaongozwa kulitafakari
Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa njia ya Neno la Mungu na kwamba, wana heri wale waliolitafakari na kulimwilisha Neno hili katika matendo. Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha mwanga unaoaangazia waamini katika hija ya maisha yao. Ni mwanga unaoyaunganisha Makanisa ya Magharibi na Mashariki na chemchemi ya furaha kwa waamini wote. Kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, ulimwengu unaweza kuuona mwanga na kuamini.

Kardinali Sandri anasema, ndugu zake Kristo ni wale wanaotekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, aliyejiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili kushiriki katika Fumbo la Ukombozi. Bikira Maria ni Hekalu na Tabernakulo ya Neno wa Mungu, mfano kwa Familia ya Mungu inayotafuta kutekeleza mapenzi ya Mungu.

Kardinali Sandri anasema, Makanisa mengi ya Mashariki yataufunga Mwaka wa Imani katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Desemba, kutokana na nafasi ya Bikira Maria katika Makanisa ya Mashariki.

Kanisa linaendelea kusali na kuwaombea wananchi wa Syria katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha yao. Katika Ibada hii ambayo imehudhuriwa na wajumbe wa Makanisa ya Mashariki na baadhi ya viongozi wandamizi kutoka Vatican, wamesali pia kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Khalifa wa Mtakatifu Petro, aliyepewa dhamana ya kuhudumia umoja katika ukweli na upendo, aendelee kutekeleza utume wake kwa ari na moyo mkuu zaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.