2013-11-21 08:32:29

Liturujia ya Kanisa ni kiini cha maisha na mahali ambapo mwamini anakutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusu Mwaka wa Imani sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican anabainisha kwamba, Mtaguso mkuu limekuwa ni jiwe kuu la pembeni katika maisha, historia na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. RealAudioMP3

Anasema, lengo kuu la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni kuhakikisha kwamba, hazina takatifu ya Mafundisho hai ya Kanisa inalindwa na kufundishwa kwa namna inayofaa zaidi, kwani ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu katika ujumla wake. Ni mafundisho yanayogusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu: kiroho na kimwili kw akuhamasisha: umoja na mshikamano; haki na amani.

Kardinali Pengo anasema, kwa upande wake hati juu ya Liturujia ya Kanisa yaani Sacrosanctum Concilium inayofafanua maumbile ya Liturujia na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa; inayohimiza malezi ya kiliturujia na ushiriki mkamilifu wa waamini; hati inayofanya marekebisho makuu katika Liturujia; umuhimu wa Sakramenti ya Ekaristi takatifu kama kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; Sakramenti, Liturujia ya vipindi na Mwaka wa Kanisa, Muziki na sanaa takatifu ni kati ya mambo ambayo yamemgusa kwa namna ya pekee kabisa.

Anasema, marekebisho yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yamewasaidia waamini kujisikia kuwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Liturujia kwa njia ya ushiriki wao makini kwa kuadhimisha na kusali katika lugha wanayoifahamu.

Kardinali Pengo anaonya kuhusu tafsiri potofu ya mabadiliko ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican katika Liturujia kwa baadhi ya waamini kudhani kwamba, wanaweza "kujifanyia" mambo kama wanavyotaka wenyewe. Kanisa linapenda kuhakikisha kwamba, waamini wanasali na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kadiri ya sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Mama Kanisa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Liturujia ni kiini cha maisha, mahali pa kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa mwamini mwenyewe.







All the contents on this site are copyrighted ©.