2013-11-21 07:48:02

Iweni mashahidi wa amani, furaha na huruma ya Mungu kwa waja wake!


Katika kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha kwa mara ya kwanza Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Francisko amewaambia Wakristo wanaoishi Nchi Takatifu kwamba, Mwaka wa Imani kimekuwa ni kipindi cha neema na baraka kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Waamini wamepata fursa ya kutafakari kuhusu Mafumbo ya Imani na Utakatifu wa Mungu, tayari kutoka kimasomaso kuwashirikisha wengine ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa waamini hao waliokutanika hivi karibuni mjini Yerusalem kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Imani Kimataifa sanjari na kuufunga Mwaka wa Imani katika Nchi Takatifu, amewapongeza kwa kulinda na kuhifadhi maeneo matakatifu kama kielelezo cha utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema hata baada ya kufunga rasmi Mwaka wa Imani, waendelee kwa ari na moyo mkuu kuwa ni mashahidi wa amani, furaha na huruma ya Mungu kwa waja wake. Anasema, uwepo wa Wakristo katika Nchi Takatifu iwe ni alama ya upendo wao kwa Kristo na Kanisa lake.

Katika Ibada ya Misa Takatifu, Patriaki Fouad Twal wa Yerusalem, amekazia umuhimu wa imani katika hija ya maisha ya waamini hapa duniani, kwani inawasaidia kuweza kutambua kweli za kiimani, ili hatimaye, kujishikamanisha na Mungu. Siku ya Imani Kimataifa ilikuwa imeandaliwa na viongozi wa Kanisa wanaotekeleza dhamana na utume wao katika Nchi Takatifu. Maadhimisho haya yalitanguliwa na tafakari ya kina kuhusu "Nchi Takatifu na Bikira Maria Mama wa Yesu. Tukio hili limehitimishwa kwa maandamano na sala kwenye Kanisa kuu la Kupashwa Habari kwa Bikira Maria kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.