Mwarobaini wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amependekeza hatua
saba za msingi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupunguza uzalishaji
wa gesijoto na kuongeza fedha za kukabiliana na hali hiyo duniani. Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa ni siri ya wazi kuwa Afrika inateseka zaidi kwa kukabiliwa na changamoto
nyingi na za kila aina kutokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ukweli kuwa
inachangia kidogo sana katika kuzalisha gesijoto na kuharibu mazingira.
Akizungumza
kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi wa COP19/CMP9
mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Poland, mjini Warsaw, Jumanne, Novemba
19, 2013, Rais Kikwete amewaambia mamia ya washiriki wa Mkutano huo kuwa dunia inahitaji
kuchukua hatua saba za msingi kukabiliana na hali hiyo.
Hatua hizo ni zifuatazo:
(a).
Kukubaliana kuhusu njia za msingi za kitaasisi za jinsi ya kuzifidia nchi kutokana
na upotevu unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi. (b). Kukubaliana kuhusu ni taasisi
ipi itasimamia shughuli zinazohusiana na misitu. Taasisi itakayohakikisha na kusimamia
namna ipi nchi masikini zinavyoweza kufidiwa kifedha kutokana na upunguzaji wa gesijoto. (c).
Kukubaliana kuhusu misingi, masharti na maelekezo ambayo yatasimamia hatua za kupunguza
gesijoto katika nchi zilizoendelea.
(d). Hatua na njia ambazo zitaongoza nchi
zilizoendelea kupunguza gesijoto zinatakiwa kukubaliwa na kuelezwa waziwazi. (e).
Kuna umuhimu wa haraka wa kuupatia Mfuko wa Mazingira wa Kijani fedha za kuanzisha
na kuimarisha Mfuko huo. Kwa sasa ni Mfuko mtupu. Lazima tuhakikishe kuwa unajazwa
ipasavyo. Aidha, lazima tukubaliane namna gani kiasi cha dola za Marekani Bilioni
100 zilizokubaliwa kuchangwa kila mwaka zitakavyopatikana na kugawanywa.
(f).
Kituo cha Teknolojia ya Mazingira na Mtandao kitafute jinsi ya kuondoa vikwazo katika
masuala yanayohusiana na uhamishaji wa teknolojia kutoka nchi tajiri kwenda nchi zinazoendelea
na kumaliza changamoto zinahusiana na Haki Miliki. (g). Kwenye COP hii tunahitaji
kukubaliana kuhusu baadhi ya mambo yanayohusiana na upunguzaji wa gesijoto.
Rais
Kikwete alikuwa anazungumza kwa niaba ya viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika nafasi
yake akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi
(CAHOSCC).
Rais Kikwete amekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo tokea Januari, mwaka
huu, 2013, wakati alipochaguliwa na viongozi wenzake kushika nafasi hiyo kufuatia
kifo cha aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Meles
Zenawi, Septemba, mwaka 2012.
Viongozi wengine ambao wamezungumza katika Mkutano
huo wa ufunguzi ambao Mwenyekiti wake alikuwa ni Rais wa COP 19 Mheshimiwa Marcin
Korolec, Waziri wa Mazingira wa Poland ni Waziri Mkuu wa Poland, Mheshimiwa Donard
Tusk na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon.
Wengine
ni Rais wa Mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Balozi John
Williams Ashe ambaye ni Balozi wa Antigua na Barbuda katika Umoja wa Mataifa na Katibu
Mtendaji wa Mkataba wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Umoja wa Mataifa
(UNFCC), Mheshimiwa Christiana Figueres.