Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa, Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi, Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania katika mahojiano na Radio Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya
Mwaka wa Imani anabainisha kwamba, Sakramenti za Kanisa zinagusa hatua zote na nyakati
zote muhimu za maisha ya Mkristo.
Zinayajalia
maisha ya ya imani ya Mkristo, kuzaliwa na kukua, kupona na utume. Sakramenti ya Ekaristi
takatifu ni "Sakramenti ya Sakramenti" inayopaswa kupokelewa na waamini waliojiandaa
kukutana na Yesu Kristo katika hija ya maisha yao, tayari kwenda kumtangaza na kumshuhudia
kwa njia ya maisha adili. Waamini wajitahidi kufanya maandalizi makini kabla ya kupokea
Sakramenti za Kanisa huku wakiwa na moyo safi. Wasikubali kuishi uchumba sugu!
Askofu
msaidizi Nzigilwa anawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuishi maisha
adili kwa kuongozwa na amri za Mungu. Watambue kwamba, sheria ya Mungu imekwisha andikwa
katika dhamiri zao, hivyo wanawajibika kulea na kuikuza dhamiri nyofu ili hatimaye,
waweze kutoa maamuzi sahii ya kimaadili, kwa kutenda mema na kuachana na ubaya. Amri
za Mungu ziwe ni dira na mwongozo wa maisha adili.